Jumatatu , 7th Mar , 2016

Zile mbio za kuwania usukani wa ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL zinataraji kuendelea tena katikati ya juma hili kwa vilabu vyote kushuka Dimbani katika mikoa na viwanja tofauti ili kuwania alama tatu muhimu na kujiimarisha katika mbio za ubingwa.

Michezo saba ya Ligi Kuu ya soka Tanzania bara (VPL) inatarajiwa kuchezwa katikati ya wiki hii, kwa kesho kuchezwa mchezo mmoja, huku michezo mingine sita ikichezwa siku za Jumatano na Alhamisi katika viwanja mbalimbali nchini.

Kesho Jumanne,mabingwa watetezi timu ya Young Africans watakua wenyeji wa Wana Kimanumanu African Sports, mchezo utakaoanza majira ya saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Jumatano Machi 09, 2016 Tanzania Prisons watakua wenyeji wa Kagera Sugar kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku Coastal Union wakicheza na ndugu zao maafande wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Mwadui FC watakua wenyeji wa Majimaji katika uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga, huku JKT Ruvu wakiwakaribisha Toto African katika uwanja wa Mabatini , Mlandizi mkoa wa Pwani.

Alhamisi hii vinara wa ligi hiyo Simba SC wao watawakaribisha Ndanda FC kutoka Mtwara katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku wagonga nyundo wa jiji la Mbeya timu ya Mbeya City wakiwakaribisha Stand United chama la wana katika uwanja wa Sokoine.