Ijumaa , 13th Mei , 2016

Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa wiki ijayo atarajiwa kutangaza kikosi cha wachezaji wake wakaokwenda Kenya kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika jijini Nairobi, Mei 29, 2016.

Kocha Boniface Mkwasa akitoa maelekezo kwa wachezaji wa Taifa Stars.

Mkwasa ambaye anasaidiana na kocha mwingine mzawa Hemed Morocco atakutana na Waandishi wa Habari za michezo nchini Mei 18, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutaja kikosi.

Pamoja na kuutumia mchezo huo kuwania kupanda katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Stars pia itautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi yake kabla ya kumenyana na Misri katika mchezo wa Kundi G kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) mwakani, utakaofanyika Juni 4, 2016 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Stars inahitaji kuifunga Misri ili kuweka hai matumaini ya kufuzu fainali hizo za Gabon 2017.

Misri inaongoza kundi hilo lenye timu tatu baada ya Chad kujitoa kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi mbili, wakati Tanzania ina pointi moja ni ya mwisho kwa sasa.

Misri itakuwa inacheza mechi yake ya mwisho Juni 2 Dar es Salaam wakati Stars itamaliza Nigeria Septemba 2 mjini Abuja.
Stars ikishinda mechi zake mbili za mwisho itafikisha pointi saba hivyo kulingana na Misri - na maana yake timu ya kwenda Gabon kutoka Kundi G itatazamwa kwa wastani wa mabao.