Jumanne , 5th Apr , 2016

Kama Tanzania itafanikiwa kuvuka vikwazo viwili vya michezo mnne ya kufuzu kwa fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 basi hilo ndilo jambo sahihi kutokea na itakuwa sifa kubwa kwa nchi badala ya kufuzu kwa kutegemea uwenyeji wa mashindano.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys Bakari Shime [kulia] na Afisa habari wa TFF Baraka Kizuguto [katikati] pamoja na mshauri wa ufundi wa Serengeti Boys Kim Paulsen [kushoto]

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 Serengeti Boys Bakari Shime ametoa wito kwa Watanzania wote kuisaidia timu hiyo na kuipa ushirikiano hasa katika kipindi hiki ambacho iko katika maandalizi ya kufuzu kwa michuano ya mataifa ya Afrika kwa vijana AFCON U17 mwakani nchini Madagascar.

Serengeti Boys inataraji kuanza kutupa karata yake ya kwanza kati ya nne zilizombele yake kwakuvaana na timu ya vijana ya shelisheli mwanzoni mwa mwezi June jijini Dar es Salaam na baadae kurudiana nao ugenini baada ya wiki mbili huo ukiwa ni mchezo wa mzunguko wa kwanza wakuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za vijana chini ya miaka 17 fainali zake zitapigwa mnamo mwaka 2017 nchini Madagascar.

Na kama ikivuka kizingiti cha mzunguko wa kwanza timu hiyo ambayo iko chini ya Shime na Nkomwa wakipata ushauri wa kiufundi toka kwa Mdenmark Kim Palsen itakuwa na kibarua pevu tena kizito kutoka kwa timu ya vijana ya Afrika kusini ukiwa ni mzunguko wa pili na wa mwisho ambapo mshindi wa jumla katika michezo yote ya nyumbani na ugenini basi ndiye anakata tiketi ya kushiriki ngarambe ya fainali hizo za Madagacsar mwakani.

Shime amesema itakuwa ni sifa ya kipekee kwa Tanzania kufuzu katika mashindnao hayo kwa uwezo wake badala ya kutegemea michuano ijayo ya mwaka 2019 ambayo tutakuwa wenyeji ndiyo tufuzu moja kwa moja kama waandaaji kitu ambacho hakitalipa sifa soka la nchi hii.

Aidha Shime amesema kama ushirikiano na sapoti kubwa timu hiyo itapata kutoka kwa Watanzania wote kwa hali na mali katika kufanikisha maandalizi ya timu hiyo basi ni wazi malengo yao kwakushirikiana na shirikisho la soka nchini Tanzania TFF yatatimia hivyo hiyo itakuwa ni sifa pekee kwa nchi hasa ikichukuliwa baada ya michuano hiyo ya Madagascar mwakani miaka miwili baadae yaani mwaka 2019 Tanzania itaandaa michuano kama hiyo na hivyo itafuzu moja kwa moja kama wenyeji kitu ambacho amesema ili kuonekana tunaweza na tuko juu kimchezo basi ni vema tukafuzu kwa miguu miwili katika michuano ya Madagascar.

Akimalizia Shime amesema uwezo na lengo la kutimiza mipango hiyo ipo ila suala pekee lakufanikisha hilo ni Watanzania kuwa na umoja na kushirikiana kwa kila hali na namna kuisaidia timu hiyo ambayo kufanya kwake vizuri ndiyo mwanzo wa kuwa na timu bora ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 20 ambayo nayo itakuwa katia mwendelezo mzuri wa kuelekea katika timu ya miaka chini ya 23 itakayoshiriki kuzufu olimpiki ya 2020 ya Japan na baadae kuwa ndio taifa Stars mpya.

Na katika kukipa makali kikosi hicho ambacho sasa kitakuwa kikiingia kambili kila baada ya wiki mbili za mwisho wa mwezi timu hiyo imefanikiwa kupata kipimo kizuri cha michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki wakicheza na timu bora ya vijana ya Misri the Pharaohs mmoja ukipigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na mwingine ukichezwa katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Kwa hali hiyo kocha Shime amesema juhudi binafsi za Watanzania kuisaidia timu hiyo badala ya kuiachia majukumu hayo TFF pekee ndiyo itakuwa suluhisho lakufuta uteja ama kuwa kichwa cha mwendawazimu na kufanya Tanzania kuwa moja ya timu za kuogopwa barani Afrika.