Jumamosi , 21st Nov , 2020

Kocha mkuu wa klabu ya Simba Mbelgiji Sven Vandenbroeck amethibitisha atawakosa wachezaji wake nyota wanne wa kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa hii leo ambapo Simba wanatazamiwa kushuka dimbani saa 10 kamili jioni hii leo kuwavaa Wagosi wakaya Coastal Union kwenye VPL.

Meddie Lagere(Pichani) akishangilia bao na kulia kwake ni Luis Miquissone ambao kwa pamoja watakosekana katika mchezo wa leo.

Nyota  wanaotazamiwa kuukosa mchezo wa hii leo ni Mshambuliaji Meddie Kagere, Chris Mugalu, Luis Miquissone na kiungo Jonas mkude kutokana na baadhi kuwa na majeraha na kupewa mapumziko baada ya akutoka kwenye michezo ya timu za taifa.

Sven anatazamiwa kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake hii leo ili kuziba nafasi za wachezaji hao wanaotazamiwa kukosekana huku kiungo Ibrahim Ajib, Said Ndemla, Mshambuliaji Charles Ilanfya na winga Miraji Athumani wakitaraji kupewa nafasi kucheza hii leo.

Licha ya kuthibitisha kuwakosa wachezaji wake nyota, Kocha Sven amesema anauona mchezo huo ni kipimo tosha kuwaandaa na mchezo unaofuata dhidi ya klabu ya Plateau Utd ya nchini Nigeria kwenye mchezo wa hatua ya awali ya mtoano kuwania kutinga makundi ya michuano ya klabu bingwa Afrika.

Kwa Upande wa kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda ambaye pia ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars' amejinasibu kuondoka na alama zote tatu mbele ya mabingwa watetezi Simba na kuwashangaza wapenzi wa soka wengi ambao hawawapi nafasi ya ushindi hii leo.

Simba wanashika nafasi ya 3 kwenye msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kucheza michezo 10, kupata ushindi michezo 6, sare 2 na kufungwa michezo 2 na kujizolea alama 20 ilhali Coastal Union wanashika nafasi ya 11, Ushindi michezo 3, sare 3 na vipigo 4 na kufikisha alama 12.

Michezo mingine itakayopigwa leo ni  Jkt Tanzania dhidi ya Gwambina, Polisi Tanzania watakabiliana na Ihefu, nayo Kmc dhidi ya Azam Fc