Kwa nini Bwalya na Mugalu hawapati nafasi Simba?

Jumatano , 16th Sep , 2020

Meneja wa kikosi cha Simba, Patrick Rweyemamu amesema ni mapema sana kuhoji kwa nini wachezaji wao wapya hawachezi katika kikosi cha kwanza kama ambavyo wengi wanaulizia hivi sasa.

Larry Bwalya baada ya kuwasili Simba.

Rweyemamu ametolea ufafanuzi huo kufuatia Kocha wa Simba, Sven Vandebroeck kutowatumia nyota wapya wakiwemo Larry Bwalya na mshambuliaji Chris Mugalu waliosajiliwa kutoka nchini Zambia jambo ambalo limeibua maswali mengi kutoka kwa wafuatiliaji wa soka nchini.

''Sidhani kama ni sawa kuhoji ni kwa nini Bwallya na Chriss Mugalu hawachezi kwa sasa ,ndio kwanza tumecheza mechi mbili pekee za ligi dhidi ya Ihefu na Mtibwa,hata wachezaji waliokuwepo msimu uliopita wakiwemo Beno Kakolanya,Fraga hawajacheza, tafadhali jamani tuwape muda.

Halafu Kocha anaendelea kutengeneza kikosi sio lazima wote wacheze kama watu wanavyotaka,kikubwa ni kupata matokeo lakini nasisitiza tuwape muda wachezaji wetu na sio kuwashinikiza''alisema Rweyemamu.

Klabu ya Simba itashuka dimbani kwa Mkapa siku ya Jumapili kuikabili Biashara United kutoka Mara mchezo ambao utawashuhudia mabingwa hao watetezi wakicheza katika Jiji la Dar es salaam kwa mara ya kwanza katika ligi tangu msimu mpya uanze kutimua vumbi.

Simba iliwasajili Larry Bwalya kutoka Lusaka Dynamos,Chriss Mugalu akitokea Power Dyamos,Ibrahim Ame kutoka Coastal Union ya Tanga,Charles Ilanfia kutoka KMC,Joash Onyango kutoka Gor Mahia ya Kenya David Kameta kutoka Lipuli na Benard Morrison kutoka Yanga.