Jumamosi , 18th Jun , 2016

Katika kuelekea shamrashamra za mashindano ya Olimpiki ambayo mwaka huu yanafanyika huko Jijini Rio Brazil familia ya mchezo wa mpira wa magongo mkoa wa Dar es Salaam wao wanafanya maadhimisho ya mashindano hayo kwa mashindano ya shule za msingi.

Baadhi ya wanafunzi wakijifunza mchezo wa mpira wa magongo

Chama cha mpira wa magongo Mkoa wa Dar es Salaam DRHA, kimeadhimisha mashindano ya michuano ya Olimpiki ya Rio Brazil kwa kwa kucheza mashindano ya mchezo wa mpira wa magogo kwa wanafunzi wa shule za msingi mkoa wa Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa chama cha mpira wa magongo mkoa Dar es Salaam DRHA Mnonda Magani amesema wanatumia mashindano hayo kuwahamasisha watoto hasa hao wa mashuleni kupenda mchezo huo huku pia wakitumia mashindano hayo ambayo yanafanyika katika viwanja vya JMK Park Kidongo Chekundi Mnazi Mmoja kuvumbua vipaji vipya kwa ajili ya timu ya vijana ya Mkoa na pia kwa timu ya taifa ya vijana ya mchezo huo.

Magani amesema mashindano hayo ya siku mbili ambayo yameanza jana na yatamalizika leo yanataraji kutimiza lengo lao la kuwapa hamasa vijana hao kutoka mashuleni kuupenda mchezo huo lakini pia wanatimiza lengo kuu la kuadhimisha Olimpiki likiwa ni agizo maalumu kwa mara ya kwanza kutoka shirikisho la michezo ya Olimpiki duniani.

Magani ambaye pia ni kocha na mkufunzi wa mchezo huo amesema pamoja na kuandaa michuano hiyo kwa mara ya kwanza kutokana na utaratibu huo mpya uliotolewa kwa vyama vya michezo yote duniani ambavyo ni wanachama wa shirikisho la michezo ya Olimpiki wao wameona ni vema kutumia fursa hiyo kuwekeza kwa vijana hasa wa mashuleni kwa kuwahamasisha kupitia mashindano ya wao kwa wao.

Akimalizia Magani amesema pamoja na changamoto mbalimbali wao kama chama wamejipanga kwa kiasi chao na kuandaa zawadi mbalimbali kwa ajili ya washindi na wale watakaofanya vizuri na kuwa bora kuliko wengine katika maeneo tofauti ambapo fainali zake zitapigwa kesho katika viwanja hivyo vya JMK Park jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kuwapa motisha watoto hao na kuwafanya waupende mchezo huo na kuwavutia wengine kwa wingi wajitokeze kujifunza na hatimaye kuucheza mchezo huo.