Alhamisi , 21st Apr , 2016

Baada ya uongozi wa chama cha makocha ama walimu wa mchezo wa kuogelea nchini TSCA kumaliza muda wao tangu mwaka jana sasa chama hicho kiko tayari kufanya uchaguzi mkuu wake ifikapo mwezi Mei mwaka huu jijini Dar es salaam.

Viongozi wa TSCA, Kutoka kulia ni Alexander Mwaipasi rais wa chama cha Makocha wa kuogelea nchini, Amina Mfaume katibu wa chama na Michael Livingstone Mkurugenzi wa Habari

Kamati kuu ya utendaji ya chama cha makocha wa mchezo wa kuogelea nchini TSCA kimetangaza na kuwajulisha wadau wa mchezo huo kuwa kinataraji kufanya uchaguzi mkuu wa chama hicho taifa mwaka huu ifikapo Mei 21.

Rais wa TSCA Alexander Mwaipasi amesema uchaguzi huo utahusisha nafasi ya Rais, katibu mkuu, katibu mkuu msaidizi, mkurugenzi wa fedha mkuu na msaidizi wake na mkurungenzi wa habari na uenezi na wajumbe wa kamati mbalimbali.

Aidha Mwaipasi amesema uchaguzi huo utasimamiwa moja kwa moja na Baraza la michezo nchini BMT na ndiko fomu za kuwania nafasi za uongozi wa chama zinapatikana katika ofisi zao zilizoko posta mpya jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa mwisho wa zoezi la uchukuaji fomu ni Mei 14 mwaka huu.

Akimalizia Mwaipasi amesema kabla yakuanza zoezi la uchaguzi mkuu huo ama kabla ya kufanyika uchaguzi huo ambao unatakiwa uanze saa 2 asubuhi na kuhitimishwa saa tano asubuhi pia kutakuwa na mkutano mkuu na mwisho akasisitiza ama akatoa wito kwa makocha wote bara na visiwani kujitokeza.