Jumatano , 31st Dec , 2014

Rais wa Chama cha Ngumi za Kulipwa nchini TPBO, Yassin Abdallah amesema anaamini pambano dhidi ya Thomas Mashali na Abdallah Mbabe litakalofanyika katika ukumbi wa Friends Corner jijini Dar es salaam, litakuwa gumu kutokana na kila bondia kujiandaa.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Abdallaha amesema pambano hilo ambalo litakuwa la raundi Nane, uzito wa kilo 70 Middle Weight amesema anawafahamu mabondia hao ambao wameshapigana hivyo anaamini kila bondia kajipanga kwa ajili ya pambano hilo.

Kwa upande wake Abdallah Mbabe amesema, anaamini atafanya vizuri kutokana na kuwa na rekodi nzuri katika mapambano mbalimbali aliyopigana.

Kwa Upande wake Thomas Mashali amesema, anajiamini na ana uwezo wa kuendelea kuwa mbabe katika pambano hilo.

Kwa upande wake Promota wa Pambano hilo, Dotto Madebe amesema, Pambano hilo linalowakutanisha mabondia waliokuwa wakitafutana kwa muda mrefu litatanguliwa na mapambano 13 kutoka kwa mabondia mbalimbali.