Alhamisi , 19th Sep , 2019

Timu ya Flying Dribblers imejipigia kifua kuwabwaga mabingwa watetezi wa michuano ya Sprite Bball Kings 2019, Mchenga Bball Stars kuelekea nusu fainali ya michuano hiyo wikiendi hii.

Flying Dribblers

Akizungumza katika mahojiano na EATV & Radio Digital kuhusiana na maandalizi yao kuelekea mchezo huo, nahodha wa Flying Dribblers, Habi Mayeye amesema kuwa wamejipanga vyema na maandalizi yananendelea kuelekea mchezo huo, huku akiwapa tahadhari kuwa wamejipanga kuwaondoa.

"Kwa misimu mitatu sasa tumekuwa tukikutana na Mchenga na bahati mbaya wametufunga mechi mbili, kwahiyo na sisi huu ni wakati wetu wa kuwafunga na kurudisha hadhi yetu", amesema.

"Sisi siku zote tunakuwaga tumepoa, ni wakimya yaani. Lakini watu wanashangaa tu tunafika nusu fainali, mimi nimegundua tuna mashabiki japo kuna timu zina mashabiki wa amsha amsha lakini sisi tunao mashabiki hao na naamini siku ya Jumamosi patawaka pale Taifa", ameongeza.

Michezo ya kwanza ya nusu fainali ya Sprite Bball Kings inatarajia kupigwa Jumamosi hii, Septemba 21 katika Uwanja wa Ndani wa Taifa ambapo mechi ya kwanza majira ya saa 10:00 jioni itazikutanisha kati ya KG Dallas na Tamaduni huku mechi ya pili ni kati ya Flying Dribblers na Mchenga Bball Stars.