Jumatatu , 26th Aug , 2019

Mabingwa watetezi wa michuano ya Sprite Bball Kings, Mchenga Bball Stars wameendeleza tambo zao mbele ya timu zingine kuelekea hatua ya 16 bora, itakayopigwa wikiendi hii.

Mabingwa watetezi, Mchenga Bball Stars

Akizungumza kwa niaba ya timu hiyo katika droo ya hatua ya 16 bora, iliyofanyika katika ofisi za EATV, nahodha wa Mchenga Bball Stars, Mohammed Yusuph amesema kuwa wao bado wapo vile vile na wana nafasi kubwa ya kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu.

"'Basketball' ni mpira wa kucheza uwanjani na hauwezi kuwa bingwa bila kucheza na timu ngumu. Mashindano ni mazuri, watu wamesajili timu zao lakini bado Mchenga ana nafasi yake palepale", amesema nahodha wa timu hiyo maarufu kama 'Mudi'.

Naye kwa upande wake, mwakilishi wa timu ya Temeke Heroes, ambao ndiyo wapinzani wa Mchenga katika hatua ya 16 bora amesema kuwa walikuwa wakiomba tangu mwanzo wa mashindano wapangiwe na Mchenga ili wawatoe mapema na ndoto yao imeshatimia, kilichobakia ni kutimiza.

Hatua ya 16 bora inatarajia kufanyika Septemba 7 na Septemba 8 katika Uwanja wa Don Bosco Oysterbay, Jijini Dar es Salaam.

Mashindano haya yanafanyika kwa msimu wa tatu yakiandaliwa na East Africa TV na East Africa Radio kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite, ambapo mshindi wa mashindano atajishindia kitita cha takribani 10 milioni.