Jumatano , 14th Aug , 2019

Mashindano ya tatu ya Sprite Bball Kings 2019 yanayoandaliwa na East Africa TV na East Africa Radio kwa kushirikiana na kinywaji cha Sprite, yanatarajia kuzinduliwa Jumamosi hii, Agosti 17 katika viwanja vya Mlimani City, Dar es Salaam.

Msimamizi wa Sprite Bball Kings 2019, Bhoke Egina

Maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa kuelekea uzinduzi wake, ambapo siku ya uzinduzi itaambatana na usajili wa timu shiriki pamoja na burudani kadhaa kwa wageni ambao watahudhuria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za EATV, Msimamizi wa Sprite Bball Kings 2019, Bhoke Egina amesema kuwa wanatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa washiriki huku akitaja zawadi ambazo zitatolewa kwa mabingwa.

"Mshindano yanatarajia kuanza siku ya Jumamosi, Agosti 17 pale Mlimani City ambapo tutaanza na usajili na tunaita timu zote kuja kujisajili kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo. Huu ni mwaka wa tatu EATV na EA Radio inaendesha mashindano haya kwa lengo la kuukuza huu mchezo kwa Watanzania kutokana na kwamba haupewi kipaumbele", amesema Bhoke.

"Timu ambayo itashinda ubingwa itapata kiasi cha shilingi millioni 10, mshindi wa pili atapata milioni tatu na MVP atapata Sh milioni 2 pamoja na vikombe vitakavyotolewa kwa washindi wote", ameongeza.

Aidha Msimamizi wa mashindano amesema kuwa vigezo vitakavyozingatiwa ni pamoja na umri wa washiriki ambao ni kuanzia miaka 16, timu shiriki zinatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 10.

Mashindano ya Sprite Bball Kings yalizinduliwa rasmi kwa mara ya kwanza Mei 3, 2017 na jumla ya timu 52 toka sehemu mbalimbali Tanzania zilijisajili.