Jumapili , 1st Mar , 2015

Zaidi ya wanachama hai wa klabu ya soka ya Simba hii leo (Machi 01, 2015) wamekutana pamoja katika mkutano wa kikatiba ambao umefanyika kwa amani na utulivu mkubwa

Baadhi ya wanachama wa klabu ya soka ya Simba wakiwa katika mkutano wa klabu hiyo hii leo.

Mkutano mkuu wa kawaida wa wanachama wa klabu ya soka ya Simba umefanyika hii leo katika ukumbi wa Bwalo la maofisa wa polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam ukiwa na ajenda tatu, ujenzi wa uwanja na mustakabali na mwenendo wa timu hiyo katika ligi.

Rais wa Klabu hiyo Evans Aveva amewaambia wanachama wa klabu hiyo kuwa hakuna mgogoro wala mgawanyiko ndani ya klabu hiyo na kinachotokea hivi sasa ni kipindi cha mpito na sababu kubwa ya timu hiyo kusuasua katika ligi kuu ni kutokana na ukata unaoikabili timu hiyo, ugeni wa kocha, uchanga wa kikosi hicho ambacho kinaundwa na asilimia kubwa ya vijana wadogo na hivyo amewataka wanachama hao kuwapa muda ili watatue changamoto hizo.

Katika masuala mengine pia uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais wake Evans Aveva ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho amesema wako katika hatua nzuri za kupata pesa za udhamini wa ujenzi wa uwanja wao utakaojengwa maeneo ya Boko jijini Dar es salaam sambamba na hostel za klabu hiyo mpango ambao upo katika moja ya mikakati mikubwa ya kuhakikisha klabu hiyo inajitegemea kiuchumi.

Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa klabu hiyo waliutaka uongozi wa timu hiyo kutekeleza yale waliyoahidi wakati wakiingia madarakani na pia kuhakikisha wanarekebisha mapungufu yote ambayo yako katika timu yao ili iweze kupata matokeo chanya ambayo wengi walikuwa wakiyategemea hasa baada ya timu hiyo kufanya marekebisho makubwa ya kikosi cha timu hiyo na benchi zima la ufundi.