Jumatano , 2nd Mar , 2016

Kocha mkuu mpya wa wagonga nyundo wa jiji la Mbeya timu ya Mbeya City Mmalawi Kinnah Phiri ametangaza kikosi cha wanandinga 18 watakaoivaa Simba siku ya Jumapili katika mchezo wa marudiano wa ligi kuu Tanzania bara VPL.

Viongozi wa timu ya Mbeya City wakiwa na kocha mkuu wa timu hiyo Mmalawi Kinnah Phiri.

Mapema leo Phiri amesema kuwa anatua jijini Dar na kikosi cha nyota hao ambao aliwaandaa maalum kwa mchezo huo wa mwishoni mwa juma akiwa na imani kubwa kuwa wataiwezesha City kuibuka na ushindi kutokana na kuiva vizuri kimazoezi na mafunzo waliyoyapata katika wiki nzima ya maandalizi .

“Nina imani nao kuwa, wamefanya vizuri sana kwenye mazoezi ya wiki hii, sina shaka na wao kutupatia matokeo kwa sababu wako sawa tayari kwa mchezo, tutacheza kwenye mfumo mpya ambao haujawahi kuonekana tukicheza, hii ni kwa sababu tumedhamiria kupata ushindi kama ambavyo timu imekuwa ikifanya kila inapokutana na Simba”, alisema.

Miongoni mwa nyota walio kwenye orodha ya kuivaa Simba siku hiyo ya Jumapili ni pamoja na mlinzi Hassan Mwasapili, mlinda lango Haningtony Kalyesubula pia wamo Temi Felix, Haruna Shamte, Yohana Moriss, Kenny Ally na wakali wengine 12 ambao wamepewa majukumu kadhaa kuhakikisha City inaandikisha pointi tatu muhimu mbele ya timu hiyo maarufu kwa jina la wekundu wa Msimbazi.

Wakati huo huo kuelekea mchezo huo kiungo mshambuliaji wa City, Ramadhani Chombo Redondo amesema mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Simba uliopangwa kuchezwa Jumapili hii kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam utakuwa mgumu kutokana na mazingira ya timu zote mbili.

Akizungumza kupitia tovuti ya klabu hiyo, Chombo amesema kuwa City inakwenda Dar kucheza mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa uliopita kama ilivyo kwa simba, jambo ambalo linaufanya mchezo huo kuwa mgumu kutokana na uhitaji wa matokeo kwa timu zote.

“Ni wazi utakuwa mgumu, hii ni kwa sababu kila timu inahitaji matokeo baada ya kupoteza mchezo uliopita,Simba na timu nzuri na wako kwenye nafasi nzuri pia lakini wasitegeme kupata ushindi kw sababu sisi tunauhitaji zaidi yao” alisema.

Aidha Chombo aliweka wazi kuwa City ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo hasa ukizingatia kuwa imekuwa na historia nzuri kila inapokutana na Simba kwenye uwanja wa Taifa.

“City imeshinda mara kadhaa mbele ya Simba, hili ni jambo nzuri kisaikolojia kwa sababu linaleta kujiamini, imani yangu kubwa dakika 90 za Jumapili zitakuwa upande wetu” alisema.