Jumatano , 11th Sep , 2019

Moja ya wachezaji wenye pointi nyingi za kufunga mpaka sasa katika michuano ya Sprite Bball Kings 2019, Baraka Mopele, ameitaja sababu iliyompelekea kuhama klabu yake ya Flying Dribblers.

Baraka Mopele

Mchezaji huyo ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Tamaduni, aliyohamia msimu huu kutoka Flying Dribblers ambayo iliyocheza fainali ya mwaka jana dhidi ya Mchenga Bball Stars amesema ilikuwa ni ahadi baina yake na timu ya Tamaduni ambayo msimu uliopita ilikuwa ikiitwa Portland.

"Nimehamia kwa sababu ilikuwa ni ahadi tu baina yetu tangu msimu uliopita kwa sababu walijaribu kunisajili kabla ya mashindano ya msimu wa 2018 kwahiyo nikawaahidi nitajiunga nao msimu huu", amesema Mopele.

Kuhusu ushindani wa mwaka huu, Mopele amesema kuwa wako kamili msimu huu na wamejipanga kushindania ubingwa. Mopele na timu yake ya Tamaduni imepangwa na Ukonga Hitmen katika mchezo wa robo fainali utakaopigwa Jumapili hii, Septemba 15 katika Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam.

Michezo mingine, Flying Dribblers itapambana na Dream Chasers, K.G Dallas ikicheza na Water Institute huku Mchenga Bball Stars ikicheza na TMT.