Jumatatu , 9th Sep , 2019

MVP wa michuano ya Sprite Bball Kings mwaka 2018, Baraka Sadick amesema kuwa nahitaji ofa ya mshahara kuanzia  Sh. milioni 15 ili ajiunge na timu ya nje ya nchi.

Baraka Sadick akiwatoka wapinzani wake katika michuano ya Sprite Bball Kings

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa hatua ya 16 bora kati ya mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars na Temeke Heroes, Jumamosi, Septemba 8 katika viwanja vya Don Bosco Oysterbay, Baraka amesema,

"Mimi ni mchezaji mkubwa, hivi karibuni tu nilikuwa katika mashindano ya Zone Five niliibuka mfungaji bora na juzi katika mashindano ya majeshi pia niliibuka mfungaji bora, nilikutana na wachezaji wakubwa wa Misri", amesema.

"Misri walikuja walikuwa wanataka kunichukua lakini mimi nilitaka mshahara wa Sh. milioni 15 kwahiyo wakasema watakuja, sasa hivi kuna mazungumzo yanaendelea kati yetu", ameongeza.

Aidha Baraka ametuma salamu kwa wapinzani wake katika hatua ya robo fainali, akisema kuwa vyovyote itakavyokuwa katika mchezo huo lakini yeye na wenzake watahakikisha wanashinda na kufika hadi fainali.

Ikumbukwe kuwa droo ya hatua ya robo fainali imepangwa hii leo, ambapo Baraka Sadick na timu yake ya Mchenga itakutana na TMT huku Tamaduni ikipangwa na Ukonga Hitmen. Flying Dribblers imepangwa na Dream Chasers huku K.G Dallas ikipangwa na Water Institute.

Michezo hiyo ya robo fainali itapigwa Jumapili hii, Septemba 15  katika Uwanja wa Ndani wa Taifa Jijini Dar es Salaam.