Jumamosi , 7th Sep , 2019

Michuano ya Sprite Bball Kings 2019 imeendelea tena leo katika hatua ya 16 bora, ambapo jumla ya michezo minne imepigwa katika viwanja vya Don Bosco Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

Matukio ya mechi za kwanza hatua ya 16 bora

Huu ni mwaka wa tatu mfululizo michuano hiyo inafanyika, ikiandaliwa na EATV na EA Radio kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite, ambapo katika michezo ya leo, jumla ya timu nne za kwanza zimepatikana zitakazoingia hatua ya robo fainali.

Mchezo wa kwanza uliowakutanisha mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars dhidi ya Temeke Heroes, imeshuhudiwa Mchenga wakishinda kwa vikapu 114 dhidi ya vikapu 93 vya Temeke Heroes, huku mchezo wa pili ukimalizika kwa Dream Chasers kuibuka na ushindi wa vikapu 109 dhidi ya 90 vya Yo! Streets.

Katika mchezo wa tatu, Tamaduni imeibuka na ushindi wa vikapu 87 dhidi ya vikapu 76 vya Nothing But Nets, huku mchezo wa nne ukimalizika kwa Water Institute kuibuka na vikapu 76 dhidi ya vikapu 70 vya Stylers.

Michuano hiyo itaendelea tena kesho saa 2:00 Asubuhi katika viwanja vya Don Bosco ambapo jumla ya michezo minne ya mwisho itapigwa kukamilisha hatua ya 16 bora. Mchezo wa kwanza, JK Ballers ballers watacheza na Ukonga Hitmen, KG Dallas dhidi ya Wagalatia, Weusi Basketball Club dhidi ta TMT na mechi ya mwisho ni kati ya Flying Dribblers na Oysterbay.