Jumatatu , 23rd Mei , 2016

Akiwa anasubiri wakati wowote atangazwe kocha Jose Mourinho tayari ameorodhesha orodha ya awali baadhi ya majina makubwa anayotaraji kuyasajili msimu ujao atakapotua Manchester United wakiwemo Zlatan Ibrahimovic, John Stones na Nemanja Matic.

Orodha ya wachezaji nyota na bei zao wanaotajwa kumfuata Mourinho Manchester United.

Wakati Mreno Jose Mourinho akijiandaa kutangazwa kama kocha mpya wa Manchester United baada ya jumatatu ya hii leo asubuhi kocha Mdachi Louis van Gaal na benchi lake la ufundi kufukuzwa tayari kocha huyo amehusishwa na usajili wa nyota wenye majina makubwa kwenye medani ya soka duniani.

Mourinho tayari ameandika orodha ya awali ya wachezaji ambao anaona watakiimarisha kikosi cha timu hiyo ambapo katika majina hayo wamo nyota wanaotikisa soka barani Ulaya kwa sasa kama Zlatan Ibrahimovic, John Stones and Alvaro Morata.

Jose Mourinho anahitaji kukiimarisha zaidi kikosi hicho cha Manchester United na kurejesha ubora wake na tayari ameanza mazungumzo na nyota kadhaa wanafasi mbalimbali zilizokuwa zikionekana kupwaya ndani ya United kama nafasi ya beki wa kati, kiungo na mshambuliaji.

Meneja huyo raia wa Ureno mwenye sifa kubwa ndani na nje ya uwanja anajiandaa kuchukuwa mikoba ya Mdachi Luis Van Gaal katika viunga hivyo vya Old Trafford.

Na tayari kuna taarifa zisizo rasmi kutoka ndani ya uongozi wa Manchester United kuwa kocha huyo anataraji kupewa kitita cha zaidi ya pauni milioni 200 ili kukamilisha zoezi hilo katika usajili ujao wa majira ya kiangazi utakaoanza Julai Mosi mwaka huu.