Alhamisi , 20th Jan , 2022

Kocha wa Manchester United Ralf Rangnick amemtetea Cristiano Ronaldo kwa kuonyesha hasira waziwazi baada ya kutolewa dakika ya 71 kwenye mchezo wa Ligi dhidi ya Brenford ambao timu hiyo imeshinda mabao 3-1. Amesema ni kawaida kwa mchezaji kufanya hivyo kama hajafunga goli.

Cristiano Ronaldo kushoto akitoka kwenye mchezo dhidi Brenford, kulia ni kocha Ralf Rangnick

Rangnick amesema sababu ya kufanya mabadiliko ya kumtoa Ronaldo na kumingiza beki Harry Maguire, mabadiliko hayo yalikuwa mahususi kwa ajili ya kuboresha safu ya ulinzi baada ya kuwa wanaongoza kwa mabao 2-0.

“Ni kawaida kwa mshambuliaji, alitaka kufunga goli. Ametoka kwenye majeraha madogo na ilikuwa muhimu kwangu kumbuka tunamchezo mwingine siku 3 zijazo. Kwa upande mwingine tulikuwa tunaongoza goli 2-0. Ni matokeo sawa na mchezo uliopita dhidi ya Aston Villa na nikaamua tulinde uongozi huo wa mabao 2-0 na ninaamini yalikuwa maamuzi sahihi.” Amesema Rangnick

Mchezo uliopita wa Ligi dhidi ya Aston Villa Manchester United waliongoza kwa mabao 2-0, mpaka dakika ya 67 kabla ya Villa kusawazisha na mchezo huo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mabao ya The Red Devils kwenye ushindi huo yamefungwa na Anthony Elanga dakika ya 55, Mason Greenwood dakika 62 na Marcus Rashford dakika ya 77 wakati bao la Brentford limefungwa na Ivan Tony dakika ya 85. Huu pia ulikuwa ni ushindi wa 300 kwa Manchester United katika viwanja vya Ugenini kwenye EPL ikiwa ndio timu iliyoshinda michezo mingi ugenini.