Jumatatu , 30th Sep , 2019

Michuano ya Sprite Bball Kings 2019 imefikia katika hatua ya mwisho ambapo hivi sasa wamebakia vigogo wawili watakaopambana kumpata mshindi.

Mchenga Bball Stars (kijani) na Tamaduni (njano)

Timu zilizoingia fainali ni mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars na Tamaduni, baada ya kushinda mechi zao mbili mfululizo za nusu fainali, ambapo Mchenga ikiiondoa Flying Dribblers na Tamaduni ikiiondoa KG Dallas.

Jumla ya michezo mitano ya fainali itapigwa, mchezo wa kwanza (Best of 5, game 1) ukianza Ijumaa, Oktoba 4 katika Uwanja wa Don Bosco Oysterbay huku mchezo wa pili ukitarajia kupigwa (Best of 5, game 2) ukipigwa Jumapili Oktoba 6 katika Uwanja wa Ndani wa Taifa, michezo yote ikitarajia kuanza saa 11:00 jioni.

Mchezo wa tatu (Best of 5, game 3) unatarajiwa kupigwa Jumanne ya Oktoba 8 katika Uwanja wa Don Bosco Oysterbay, ambapo mchezo huo utapigwa kuanzia saa 10:00 jioni. Endapo timu moja itashinda mechi zote tatu, itakuwa bingwa wa michuano hiyo na endapo matokeo tofauti na hayo yatapatikana, ratiba ya mechi zilizobaki itapangwa.

Swali moja ambalo halina jibu mpaka sasa ni je, nani ataibuka na kitita cha Shilingi milioni 10?, ni jambo la kusubiri.