Ijumaa , 24th Sep , 2021

Miamba ya mchezo wa kikapu , Savio Basketball club na Army Basketball Club 'ABC' zitashuka kwenye uwanja wa Don Bosco saa 1:30 usiku wa leo Septemba 2021 katika uwanja wa Don Bosco Oysterbay kumenyana katika game 2 fainali ya ligi ya mkoa Dar es salaam 'RBA'.

Nyota wa Savio, Hasheem Thabeet akiwa anakipiga kwenye moja ya mchezo wa mtoano kabla ya fainali.

Kuelekea mchezo wa leo Savio wapo mbele baada ya kutangulia kwenye mchezo wa kwanza kati ya ile mitano ya fainali, baada ya kushinda kwa alama 82-73 Jumatano ya Septemba 22 mwaka huu.

Mchezaji bora wa ligi ya Taiwan 'MVP'  msimu uliopita, Hasheem Thabeet, aliongoza kwa pointi 35, ribaundi 15, usaidizi 4, ulinzi wa pointi 4, na kuifanya timu yake ya Savio kuwa na matumaini wa kunyakuwa ufalme wa Dar es salaam msimu huu.

Kwa upande wa wanawake timu inayopigiwa chapua kuchua kutwaa ubingwa msimu huu, JKT Stars itashuka uwanjani leo kuchuana na VBQ katika fainali ya pili.

Mchezo wa kwanza JKT waliendelea kuonesha ukali wao baada ya kuitwanga VBQ kwa pointi 80-74 huku nyota wao Jesca Julius akifunga pointi 34 pamoja na usaidizi wa pointi 6.