Jumapili , 20th Sep , 2015

Ile kauli ya viongozi wa klabu ya Simba kutumia msemo ule wa biashara asubuhi umethibitishwa hii leo baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa tatu mfululizo katika michezo ya ligi kuu ya soka Tanzania bara ambayo inaendelea hivi sasa hapa nchini

Mshambuliaji hatari wa Simba Mganda Hamis Kiiza akishangilia moja ya mabao yake.

Mshambuliaji hatari wa klabu ya Simba Mganda Hamisi Kiiza ambaye mashabiki humwita Diego, hii leo ameifungia Simba mabao yote matatu [hat trick] katika ushindi wa bao 3-1 ambao timu hiyo uliupata katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kwakuizamisha Kagera Sugar toka Bukoba mkoani Kagera.

Kiiza amefunga hat trick hiyo leo wakati Simba ikicheza mechi yake ya tatu ya Ligi Kuu Bara nakumfanya mshambuliaji huyo aliyewahi kuichezea Yanga kufikisha mabao matano katika mechi tatu walizokwisha cheza mpaka sasa.

Simba ambayo imerejea nyumbani jijini Dar es Salaam baada ya kuwepo jijini Tanga kwa wiki moja ikicheza michezo miwili ya ligi hiyo dhidi ya timu za Afrikan Sports ambao walishinda bao 1-0 likifungwa na Hamis Kiiza na mchezo mwingine dhidi ya wagumu maafande wa Mgambo Shooting nakushinda bao 2-0 huku Kiiza tena akiifungia Simba bao 2 na la ushindi baada ya awali Mzimbabwe Justice Majadvi kufunga bao la kwanza.

Katika mchezo huo wa leo dhidi ya Kagera Sugar inayonolewa na kocha Mzawa Mbwana Makata timu ya Simba inayonolewa na kocha Mwingereza Dylan Kerr ilicheza vizuri katika kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupata bao moja lililodumu hadi mapumziko.

Bao la pili la Kiiza na kwa Simba hii leo alilifunga katika dakika ya 46 na la tatu akilifunga kunako dakika ya 90 ya mchezo huo nakuiwezesha Simba kupata ushindi huo mujarabu unaowafanya kujikusanyia alama tatu muhimu na kufikisha pointi 9 sawa na Yanga inayoongoza ligi hiyo na Azam FC ambao nao hii leo wameshinda bao 1-0 ugenini huko mwadui dhidi ya Mwadui pamoja na Mtibwa Sukari ambayo nayo ina pointi 9 baada ya hii leo kuwalaza Ndanda FC kwa bao 2-1 huko Manungu.

Goli pekee lakufutia machozi kwa timu ya Kagera Sugar likifungwa na mshambuliaji wao hatari Mbaraka Yussuf kunako dakika 80 ya mchezo huo.

Simba sasa itashuka dimbani tena Jumamosi ijayo kuwavaa mahasimu wao wakubwa na watani wao wa jadi katika soka hapa nchini mabingwa watetezi wa ligi hiyo vijana wa muholanzi Hans Van Der Pluijm timu ya soka ya Yanga, mechi inayotarajiwa kuwa ya kukata na mundu ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa mno na mashabiki wa timu hizo mbili kote nchini.