Jumamosi , 13th Feb , 2016

Hatimaye mara baada ya misimu mitatu kupita klabu ya soka ya Simba ambayo iliandamwa na migogoro ya ndani na kupelekea kufukuza makocha wanane kwa misimu hiyo mitatu sasa hali hiyo chini ya mganda Mayanja imeanza kufutika rasmi kwa matokeo ya sasa.

Mabao mawili ya mshambuliaji mganda, Hamisi Friday Kiiza [Diego] yametosha kuipa Simba SC ushindi wa bao 2-1 dhidi ya wenyeji, Stand United katika mchezo wa mkali wa ligi kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Kwa ushindi huo, Simba SC inapanda kileleni mwa ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, ikifikisha pointi 45, baada ya kucheza mechi 19, ikiwazidi kwa pointi mbili, mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi.

Aidha, Simba SC watalazimika kuiombea ‘dua mbaya’ Azam FC katika mchezo wake wa kesho dhidi ya Coastal Union uwanja wa Mkwakwani, Tanga iendelee kubaki kileleni.

Azam FC itaingia kumenyana na Coastal kesho, ikiwa na pointi 42 ikimaanisha kuwa wakishinda kwa wastani mzuri wa mabao watarejea kileleni.

Kiiza alifunga mabao yake katika dakika za 34 na 47, hivyo sasa anaongoza kwa kufunga ligi kuu akifikisha mabao 16 dhidi ya 14, ya mshambuliaji wa mahasimu wao, Yanga SC, Mrundi Amissi Tambwe.

Stand United ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 90 kupitia kwa David Ossuman.

Hata hivyo, kama Simba itashinda mechi yake dhidi Yanga wikiendi ijayo, maana yake itakuwa ni mbio kali za kileleni kati ya Simba na Azam FC na kuiacha Yanga.

Mechi nyingine za ligi kuu leo, katika dimba la karume jijini Dar es Salaam wenyeji JKT Ruvu wametoshana nguvu na Kagera Sugar kwa sare ya bao 1-1.

Katika dimba la Sokoine jijini Mbeya wenyeji Mbeya City wamewavurumisha wanakishamapanda Toto Africans ya Mwanza kwa bao 5-1 , Mkwakwani Tanga wenyeji Mgambo Shooting waliangukia pua baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 toka watanga wenzao African Sports.

Na katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara wenyeji wanakuchele Ndanda FC wamewazamisha wanalizombe majimaji ya Songea kwa kichapo cha bao 1-0.

Ligi hiyo inataraji kuendelea tena hapo kesho kwa michezo miwili kupigwa katika viwanja tofauti, huku kila timu ikisaka point tatu muhimu ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Mjini Shinyanga wenyeji wachimba migodi , Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Mwadui Complex, huku Coastal Union wakiwaalika Azam FC kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Wakati huo huo mara baada ya kuhitimishwa kwa michezo ya mwisho ya makundi ya ligi ya soka daraja la kwanza Tanzania bara na kuibuka utata wa matokeo ya michezo iliyohusisha timu zilizokuwa zikiwania nafasi ya kupanda daraja kwenda ligi kuu Tanzania bara shirikisho la soka nchini limefanya maamuzi yafuatayo kabla yakutangaza nani kapanda.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) halitatangaza timu iliyopanda Ligi Kuu msimu ujao kutoka Kundi C, mpaka itakapoamuliwa na vyombo husika vya TFF baada ya michezo ya kundi hilo kuchezwa leo jioni katika viwanja tofauti nchini.

TFF imefikia hatua hiyo ili kupata nafasi ya kupitia taarifa za michezo kati ya JKT Kanembwa v Geita Gold na Polisi Tabora v JKT Oljoro iliyochezwa leo jioni katika mikoa ya Kigoma na Tabora.

Taarifa za michezo hiyo kutoka kwa wasimamizi husika na vyanzo vingine vinakusanywa ili zifanyiwe kazi na vyombo husika vya TFF.

Katika michezo hiyo ya leo, Geita iliibuka na ushindi wa mabao 8 – 0 dhidi ya JKT Kanembwa, huku Polisi Tabora wakiibuka na ushindi wa mabao 7 – 0 dhidi ya JKT Oljoro.