Jumanne , 14th Sep , 2021

'Sports Countdown' ya leo Septemba 14, 2021 inakupitisha kuzihesabu zile stori sita klai za kimichezo, Emma Raducanu awa bilionea baada ya ushindi wa kombe la michuano ya US Open, Edinson Cavani, Ng'olo Kane, Christian Pulisic, Aguero na Ansumane Fati kukosa mchezo wa UEFA Champions League

Mshindi wa michuano ya Tennis US Open, Emma Raducan akiwa ameshikilia kombe lake.

6 - Ni wiki ambazo mshambuliaji tegemezi wa klabu ya Azam, Prince Dube Mpumelelo anatazamiwa kuwa nje ya uwanja kujiunguza baada ya kufanyiwa upasuaji tarehe 9 Septemba mwaka huu katika Hospitali ya Vicent Pelloti jijini Cape Town, Afrika kusini na kufanikiwa kurejea nchini salama Alfajiri ya Jana Septemba 13.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Azam, Zacharia Thabiti amesema Dube alikuwa anapata maumivu makali kwenye maeneo ya chini ya kitovu kushoto pindi akijaribu kukimbia kwa kasi hivyo wanaimani kubwa tatizo hilo litapona na Dube kurejea kwenye utimamu wake wa kawaida.

Mbali na taarifa ya Dube, Zacharia Thabit amethibitisha kuwa, mchezo wao wa marudio wa hatua ya awali ya mtoano kuwania kufuzu Makundi ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Horseed ya Somalia utachezwa kwenye uwanja wa Chamazi na sio Uhuru tena, na hii ni mara baada ya Horseed wenye kuchagua hvyo.

5 - Ni idadi ya timu alizozichezea Cedric Ceballos kwenye ligi ya kikapu nchini Marekani NBA kabla ya kustaafu miaka 10 iliyopita. Timu hizo ni Phoenix Suns, Los Angeles Lakers, Dallas Mavericks, Detroit Pistons na Miami Heat.

Cedric Ceballos alizua taharuki juu ya afya yake nchini Marekani baada ya wengi kuwa na hali ya sintofahamu. Cedric amevunja ukimya usiku wa kuamkia leo kupitia akaunti yake ya IG kwa kupost picha ikionesha anatumia vifaa maalum vya kupumulia na akithibitisha kuwa amepona Covid-19 baada ya kuwa hoi kwenye chumba cha uangalizi maalum ICU kwa siku 10.

4 - Ni siku zilizopita tokea Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Pope afariki dunia Septemba 10, 2021 alipokuwa anapatiwa matibabu kwenye hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuagwa jana na watu mbalimbali kwenye viwanja vya Karimjee, Posta jijini Dar, Zacharia Hans Pope anataraji kuagwa tena Asubuhi ya leo na Familia yake pekee na baadae mchana Mwili wake utasafarishwa kuelekea Mkoani Iringa ambapo mazishi yake yatafanyika huko, Eneo la Kihesa Mkimbizi.

Aendelee kupumzika kwa Amani. Amen.

3 - Ni idadi ya miaka iliyopota tokea bondia Anthony Joshua wa England ampige bondia Andy Ruiz JR wa Mexico na kufanikiwa kutetea mikanda yake ya pambano la uzito wa juu wa Dunia ya WBA, IBF, WBO na IBO katika pambano lililofanyika mji wa Diriyah, Saudi Arabia 2019.

Mbabe huyo wa kutoa dozi neno amesema kwasasa amefikia kwenye kiwango cha juu katika maisha yake ya masumbwi lakini ili azidi kuweka historia zaidi na zaidi basi hana budi kupigana na mabondia wenye uwezo wa juu na kutamka kutaka kuzichapa na Muingereza mwenzake Tyson Fury baada ya pambano lake na Oleksandor Usyk wa Ukraine Septemba 25 mwaka huu kwenye ulingo uliopo kwenye uwanja wa Tottenham Hotspurs, England na kutaraji kuwa na watazamaji 60,000 walioketi.

Anthony Joshua na Oleksandor Usyk watapigana kugombania mikanda ya uzito wa juu wa Dunia ya WBA, IBF, WBO na IBO.

2 - Ni idadi ya michezo itakayoanza kucheza usiku wa mapema ya leo Septemba 14, 2021 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kwa msimu mpya wa mwaka 2021-2022, michezo hiyo ni Young Boys (Uswizi) vs Manchester United (England) kutoka kundi F na Sevilla vs Salzburg (Austria) kutoka kundi G ambazo zote zitachezwa saa 1:45 Usiku wa leo.

Manchester United wanataraji kumkosa mshambuliaje wake Edinson Cavani aliyepata maumivu ya kifundo cha mguu na kutaraji kuwa nje kwa wiki moja au zaidi ilhali CR7 amesafiri na kikosi hadi Uswizi tayari kwa ajili ya kuleta mabalaa.

Michezo mingine itakayochezwa usiku wa leo ni 6 amabayo yote itachezwa saa 4:00 usiku. Kundi E Barcelona (Hispania) itacheza na Bayern Munich (Ujerumani) bila ya Washambuliaji wake Martin Braithwait aliyefanyiwa upasuaji wa goti,  Ansu Fati na Sergio Aguero wakusumbuliwa na kifundo cha mguu. Dynamo Kyiv (Ukraine) itakipiga na Benifica (Ureno).

Kundi E, Villareal dhidi ya Atalanta. Kundi F, Lille itachuana na Wolfsburg. Kundi H, Mabingwa watetezi Chelsea (England) watacheza na Zenit St.Petersburg bila kiungo bora wa Ulaya Ng'olo Kante na Christian Pulisic wanaosumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu ilhali Malmo (Sweeden) itacheza na Juventus.

1 - Ni nafasi anayoishikilia mwanadada, Emma Raducanu katika viwango vya ubora vya mchezo wa tennis nchini England na kumpiku Johanna Konta baada ya Raducanu kumfunga Leylah Fernandez wiki iliyopita na kuwa bingwa wa US Open kwa mara ya kwanza.

Baada ya ubingwa huo wa kihistoria kwa Raducanu, mwanadada huyo mwenye miaka 18 amepanda rasmi kwenye viwango vya ubora vya mchezo huo kutoka nafasi ya 150 hadi sasa nafasi ya 23 duniani na ya kwanza England kwa upande wa wanawake na makamu bingwa wa US Open, Leylah mwenye miaka 19 na yeye amepanda kutoka nafasi ya 73 Duniani hadi nafasi ya 28 kwasasa baada ya kufika fainali hiyo.

Emma Raducanu amejizolea paundi Milion 1.3 za England sawa za bilioni 300 na milioni 600 za Kitanzania kwa kuwa bingwa wa michuano ya US Open.