Jumatano , 31st Dec , 2014

Mashindano ya Taifa Cup yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi hapo kesho na kukamilika Januari 10, uwanja wa Sigara jijini Dar es salaam kwa kushirikisha timu 14 kutoka mikoa ya Dodoma, Pwani, Mwanza, Mara, Katavi, Arusha, Zanzibar na timu wenyeji Dar.

Akizungumza na East Africa Radio, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Netball nchini, Anna Kibira amesema kwa mara ya kwanza wamealika timu kutoka Zanzibar ambapo ipo mikoa miwili kutoka Zanzibar huku Dar es salaam ikiwa na timu kutoka Temeke ambao ni Mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Kinondoni na Ilala.

Kibira amesema maandalizi ya mashindano hayo yameshakamilika ikiwemo uchaguzi wa waamuzi ambapo timu shiriki zinatarajiwa kuanza kuingia leo huku baadhi ya timu zikichelewa kuwasili kutokana na matatizo ya usafiri.

Kibira amesema ratiba ya michuano hiyo inatarajiwa kupangwa, timu zitakapowasili zote, ambapo michuano hiyo itafunguliwa na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Mkoa wa Temeke ambao itacheza na timu itakayopigiwa kura na kutakuwa na mchezo mmoja katika siku ya Kwanza ya michuano hiyo.