Jumatano , 13th Mei , 2015

Kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinaondoka leo kuelekea Afrika kusini kushiriki COSAFA huku kikiwaacha wachezaji tisa kati ya 28 walioitwa kambini na kocha wa timu hiyo Martin Nooij.

Akizungumza jijini Dar es salaam, daktari mkuu wa kikosi hicho Billy Haonga amesema, wachezaji waliobaki nchini ni wale waliofanyiwa vipimo na kukutwa bado ni wagonjwa na watabaki wakiendelea na matibabu na mazoezi madogo madogo.

Haonga amesema waliokutwa wagonjwa katika kikosi hicho ni Nadir Haroub Canavaro, Kelvin Friday, Aishi Manula, Haruna Chanongo na Isihaka Hassan na Salum Telela huku Kiemba akiwa na ruhusa ambapo Kelvin Yondani hakufika kambini.

Haonga amesema wachezaji ambao hawatasafiri wataendelea na mazoezi wataanza mazoezi chini ya kocha mwingine akiwa anawaangalia kwa ajili ya michuano mingine.

Wachezaji watakaokuwa katika msafara ulioitwa na kocha Nooij ni makipa; Deogratius Munish ‘Dida’ (Yanga) na Mwadini Ali (Azam), mabeki ni Shomary Kapombe, Joram Mgeveke, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Oscar Joshua, Abdi Banda, Salim Mbonde na Haji Mwinyi.

Wengine ni viungo; Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Said Juma, Hassan Dilunga, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto.

Washambuliaji ni Ibrahim Hajib, Mrisho Ngasa, Saimon Msuva, John Bocco na Juma Luizio.