Jumamosi , 11th Jul , 2015

Timu ya Taifa ya Tanzania ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 (Tanzanite) hii leo imeshuka dimbani uwanja wa Azam Complex kucheza na timu ya Taifa ya Zambia chini ya miaka 20 (Young She-Polopolo).

Wachezaji wa Tanzanite ya Tanzania na Young ShePolopolo ya Zambia wakichuana.

Tanzanite imepoteza mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa fainali za wanawake za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Papua New Guinea, kwa kichapo kizito cha bao 4-0 nyumbani katika mchezo uliochezeshwa na waamuzi kutoka nchini Sudan.

Ilikuwa huzuni kwa watanzania wote waliojitokeza Uwanja wa Azam complex, Chamazi wakiongozwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi namna ambavyo Tanzanites walivyonyanyaswa na mabinti wenzao shupavu wa Zambia.

Tanzanites inayofundishwa na mzalendo, Rogasian Kaijage leo ilizidiwa kabisa na She-polopolo Uwanja wa Azam na kujikuta hadi mapumziko ikiwa tayari imekwishabugizwa 3-0.

Mabao ya Shepolopolo yalifungwa na Memory Phiri dakika ya nne, Irene Lungu dakika ya 20 na Barbara Banda dakika ya 33.
Kipindi cha pili, Zambia walirudi na moto wao tena na kufanikiwa kupata bao la nne, mapema tu dakika ya 50 kwa penalti kupitia kwa Marry Wilombe.

Refa Batouli Ibrahim wa Sudan alitoa penalti hiyo baada ya Anastazia Anthony kumfanyia faulo mshambuliaj wa Zambia, Memory Phiri.

Sasa Shepolopolo inatakiwa kwenda kushinda mabao 5-0 ugenini ili kusonga mbele.

Kikosi cha Tanzania; Najjiat Abbas, Zuwena Aziz, Happiness Hezron, Maimuna Hamisi, Anastazia Anthony, Donisia Daniel, Hamisa Athumani, Neema Paulo, Asha Shaaban Hamza/Janet Cloudy dk40, Shelider Boniphace na Stumai Abdallah.

Zambia; Hezel Natasha Nali, Mary Wilombe/Osala Kaelo dk75, Margaret Belemu, Martha Tembo, Mlika Limwanya, Lwendo Chisamu, Esther Mukwasa, Irene Lungu, Grace Chanda, Barbara Banda na Memory Phiri/Agnes Musesa dk 83.

Mechi ya marudiano itafanyika wiki mbili zijazo jijini Lusaka nchini Zambia na mshindi wa jumla kwa michezo yote miwili atasonga mbele katika hatua inayofuata.