Ijumaa , 11th Mar , 2016

Baada ya kufanya vizuri na kuibuka washindi wa pili nyuma ya Morocco katika mashindano ya kimataifa ya wazi ya Nairobi nchini Kenya mwishoni mwa juma lililopita timu ya Taifa ya Tenisi ya Tanzania ya walemavu imealikwa kwenda Japan

Wachezaji wa mchezo wa tenisi kwa walemavu wakipeana mkono katika moja ya michezo yao.

Timu ya Taifa ya mchezo wa Tenisi kwa walemavu ya Tanzania inayotumia Baiskeli ya magurudumu matatu inataraji kushiriki michuano dunia kwa walemavu ambayo itapigwa nchini Japan mwezi mei mwaka huu.

Kwa mujibu wa kocha mkuu wa timu ya Tanzania Riziki Salumu amesema pamoja na kufanya vizuri kwa timu zote mbili kwa upande wa Wanaume na Wanawake ni timu ya Wanaume pekee ambao ndiyo imalikwa rasmi kushiriki michuano hiyo mara baada ya shirikisho la dunia ITF kutuma ujumbe unaosema utawaalika kushiriki michuano hiyo mikubwa.

Riziki amesema kwa sasa mchakato wa kualikwa unaendelea na kinachosubiriwa ni kumalizika kwa michuno ya kanda zingine ambazo bado mpaka sasa ziko katika michuano mbalimbali ya kupata timu bora ambazo zitashiriki michuano hiyo toka kanda hizo.

Aidha Riziki amesema kuwa Pamoja na kukabiriwa na changamoto za ukosefu wa vifaa hasa Baiskeli Maalumu na udhamini wa mambo mbalimbali ikiwemo pesa za maandalizi kwa timu hiyo wao bado wanaendelea kujipanga kwa kufanya mazoezi kila siku huku wakingojea barua rasmi ya mualiko kutoka ITF shirikisho la kimataifa la mchezo wa tenisi duniani.

Riziki ametoa wito kwa Watanzania na wapenda michezo kote nchini na wadau wote na makampuni kuisaidia timu hiyo katika maandalizi na safari ili kuiunga mkono timu hiyo hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo timu ambayo inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa inayoshiriki.