Alhamisi , 26th Mar , 2015

Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF limesema ligi kuu ipo chini ya TFF na kamati ya utendaji ya TFF ndio yenye mamlaka ya kutunga sheria na kanuni na hata maamuzi yakishafanyika hayawezi kutenguliwa hata na FIFA.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Celestine amesema, Klabu ya Yanga imekuwa ikilalamika bila kujua ya kuwa matatizo ya TFF yatasuluhishwa hapahapa nchini na huko nje hakuna jibu watakalopata kuhusiana na mabadiliko ya kanuni hiyo.

Mwesigwa amesema, kila mdau wa Soka mwenye tatizo anatakiwa kuliwasilisha TFF na sio kuongea nje ya muhusika na tatizo la mdau mmoja lisiwe tatizo la wadau wote kwani ligi ina vilabu 14 na vinashiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa hiari.

Mwesigwa amesema, kila anayeshiriki kwenye ligi anatakiwa kusaini kwamba atatii maaamuzi na utaratibu uliowekwa na TFF au Bodi ya Ligi hivyo Klabu ya Yanga malalamiko yake yapelekwe kwa wahusika waliobadili kanuni hizo.