Alhamisi , 19th Jun , 2014

Shirika la kutetea haki za watoto la Plan International limeingia ubia na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini

Rais wa TFF Jamal Malinzi na mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jorgen Haldorsen wakisaini makubaliano ya kampeni ya afya kwa mtoto wa kike

Kwa lengo hilo, mkataba wa ushirikiano umesainiwa leo katika ofisi za makao makuu ya TFF jijini Dar es Salaam baina ya Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jorgen Haldorsen na Rais wa TFF, Jamal Malinzi. Ushirikiano huo unalenga kufanya kazi pamoja katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni.

Kwa mujibu wa Haldorsen, mchezo wa mpira ndio unaoongoza nchini na kote duniani kwa kuwa na ushabiki mkubwa na kwamba joto kali juu ya Fainali za Kombe la Dunia linaloendelea Brazil ni ushahidi tosha

Kwa upande wake, Rais wa TFF, ambaye ni mjumbe katika Kamati ya Huduma kwa Jamii ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni- FIFA, alisema kuwa ubia huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za huduma kwa jamii ya TFF na kwamba wana furaha kushirikiana na Plan International kwa lengo hili muhimu.

“Ushirikiano huu ni muhimu sana kwetu kwani unakileta chombo kikubwa kabisa cha michezo hapa nchini pamoja na shirika la Plan International hususan kwa ajili ya haki za mtoto wa kike. Tunategemea kutumia mtandao wetu nchi nzima kuelimisha juu ya usawa wa kijinsia na uhamasishaji wa haki za mtoto wa kike,” alisema Rais Malinzi.