Jumapili , 19th Jun , 2016

Mshambulaji hatari wa timu ya taifa ya Chile Eduard Vargas akicheza kwa kiwango bora ameiongoza timu yake hiyo kuipa kipigo kizito timu ya Mexico ya kina Chicharito katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Copa Amerika huko nchini Marekani

Mshambulaji hatari wa timu ya taifa ya Chile Eduard Vargas.

Mexico ambayo katika mchezo wa hii leo imecheza kiwango kibovu kabisa na kupoteana katika muda wote wa mchezo huo nakujikuta ikiadhibiwa kwa makosa yake nakupokea kichapo cha paka mwizi cha bao 7-0 kutoka kwa Chileo ambayo leo wamecheza mchezo wa hali ya juu na wakijiamini katika muda wote wa mchezo huo.

Mwiba katika mchezo huo kwa Wanamexico alikuwa ni mshambuliaji Eduardo Vargas ambaye alipachika mabao manne nakuivusha timu hiyo katika nusu fainali ambapo sasa wanataraji kuvaana na timu ngumu ya taifa ya Colombia.

Katika mchezo huo wa leo magoli mengine ya Chile ambayo leo ilikuwa bora kiwanjani katika kila idara yalifungwa na kiungo galacha Arturo Vidal na mengine mshambuliaji Alexis Sanchez na kuwafanya Wamexico kulia na kipa wao Guillhermo Ochoa katika mchezo huo uliopigwa huko katika mji wa Santa Clara.

Kipigo hicho kiliwafanya mashabiki wa Mexico kulalama wakipaza sauti 'Ole!' wakati Chile wakicheza pasi za kimadaha na ufundi na mbwembwe nyingi. 

Mbinu hiyo ya Chile kucheza mpira kwa pasi nyingi za madaha na mbinu pamoja na mbwembwe zikawazima kabisa Mexico na hivyo kuwafanya mashabiki wa Mexico zadi ya elfu 70 waliokusanyika uwanjani kuigeuka timu yao na kuanza kuwazomea kutokana na kiwango duni walichoonyesha katika mchezo mchezo huo.

Mashindano haya Copa América Centenario ni mahsusi kusheherekea Miaka 100 ya Copa America, Mashindano ya Shirikisho la Soka la Nchi za Marekani ya Kusini, CONMEBOL, ambayo yalianzishwa Mwaka 1916.

Hii ni mara ya kwanza kwa michuano hii kuchezwa nje ya Marekani ya Kusini.

Haya yatakuwa ni Mashindano ya 45 kufanyika na kawaida yake hufanyika kila baada ya Miaka Minne lakini safari hii CONMEBOL na CONCACAF, Shirikisho la Soka la Nchi za Marekani ya Kaskazini, Kati na Nchi za Visiwa vya Caribbean, walikubaliana kuandaa Mashindano maalum.

Safari hii michuano hii itakuwa na Nchi 16, badala ya 12 za kawaida, kwa kushirikisha Nchi 10 kutoka CONMEBOL na 6 za CONCACAF.

Kawaida Mshindi wa Copa America huiwakilisha Marekani ya Kusini kwenye Mashindano ya FIFA ya Kombe la Shirikisho lakini Mshindi wa Copa América Centenario hatapewa hilo kwani Mwaka Jana Chile, wakiwa Nyumbani kwao, ndio walitwaa Copa America ya kawaida na wao ndio watashiriki Mashindano ya FIFA ya Kombe la Shirikisho Mwakani, 2017, huko Urusi.