Alhamisi , 8th Jan , 2015

VILABU vya Soka nchini vimetakiwa kuacha tabia ya kuchukua magoli kipa kutoka nje ya nchi bila kuangalia na kutumia vipaji vilivyo ndani ya nchi.

Akizungumza na East Africa Radio, Kocha wa Magolikipa wa kituo cha kukuza vipaji vya magolikipa Tanzania TGC, Manyika Peter amesema magolikipa wenye vipaji na uwezo wa kufanya kazi wapo wengi hapa nchini isipokuwa wanakosa timu za kuonyesha vipaji vyao.

Manyika amesema, iwapo viongozi wa vilabu hivyo watazingatia vipaji vya magolikipa wa ndani ya nchi, watasaidia vijana hao kuweza kupata ajira pamoja na kuweza kuitangaza nchi vizuri katika michezo kwani watakuwa ni wazawa na watakuwa na uchungu na nchi yao hivyo kupelekea kufanya vizuri.

Kwa upande wake, Mlinda mlango wa Klabu ya Yanga, Juma Kaseja amesema vijana hapa nchini wenye uwezo wanatakiwa kujitokeza ili kuweza kukuza vipaji vyao ambavyo vina uwezo kuwasaidia katika maisha kiujumla.

Kaseja amesema, vijana wengi wamekuwa waoga hususani katika suala la kujifunza bila kujua ya kuwa hakuna aliyezaliwa anajua na kila mtu anafundishwa na baadaye anakuwa na uelewa wa kila alichofundishwa.