Alhamisi , 9th Oct , 2014

Baada ya Kamati ya Nidhamu ya TFF kumwandikia barua ya wito wakili anayevitetea vilabu katika mvutano wa kupinga makato ya asilimia Tano za pesa za wadhamini, hii leo Wakili huyo ameshindwa kuudhuria kikao hicho kilichofanyika hii leo

Wakili wa vilabu vya ligi kuu ya soka Tanzania bara Dr. Damas Ndumbaro pichani [kulia]

Sakata la mvutano wa makato ya alisimia 5% ya fedha za wadhamini kati ya vilabu na shirikisho la soka nchini TFF limechukua sura mpya baada ya wakili anayewakilisha vilabu vya soka vya ligi kuu na Daraja la kwanza Tanzania bara Dr. Damas Ndumbaro ambaye hii leo alitakiwa akahojiwe na Kamati ya Nidhamu ya shirikisho la soka nchini TFF kushindwa kuhudhuria kikao hicho kutokana na sababu mbalimbali.

Ndumbaro amesema miongoni mwa sababu hizo ni yeye kuwa na safari ya nje ya nchi ambayo aliipanga miezi mitatu iliyopita hivyo isingekuwa rahisi kwake kuahirisha safari hiyo na pili ni barua ya wito aliyopokea kutoka TFF inayomtaka akajibu tuhuma ambazo hazijui kwamba haikifafanua ama kueleza makosa ambayo anatakiwa akayajibu na imekuja mda mchache kabla ya kikao hicho kufanyika.

Ndumbaro amesema ni kweli amepokea barua hiyo ambayo inaonyesha iliandikwa juzi Jumanne [Oct 7] na jana akaipokea lakini kimsingi barua hiyo kisheria inamapungufu mengi na pia ameshangazwa kwa kitendo cha Kamati ya Nidhamu kumshitaki wakili anayetetea mteja wake.

Ndumbaro amekwenda mbali zaidi na kusema ameshagundua hila au mipango michafu ya baadhi ya viongozi wa TFF wenye maslahi yao na makato hayo ndio maana wanataka kumvunja moyo katika kutetea haki za mteja wake ambao ni vilabu.

Akimalizia Ndumbaro amesema kamwe hatakatishwa tamaa na hali hiyo na ataendelea kusimamia haki ya mteja wake [vilabu] mpaka ipatikane na ameshangazwa na kusikitishwa na kitendo cha shirikisho la soka nchini TFF kukaidi maagizo ya Naibu Waziri wa habari vijana utamaduni na michezo ambaye alilitaka shirikisho hilo kuangalia kwa umakini uamuzi wake juu ya sakata hilo na pia kufanya uwezekano wa kukutana na bodi ya ligi [TPLB] pamoja na vilabu na wakili wao ili kuzungumza na hatimaye kupata jawabu la kumaliza mvutano huo.