Jumamosi , 21st Jun , 2014

Uongozi wa klabu ya Yanga umesema kama idadi ya wanachama wa klabu hiyo wanaopinga maazimio ya mkutano mkuu wa klabu hiyo wa June mosi wakifikia idadi ya wanachama zaidi ya elfu moja mia tano [1500] basi watabadili maamuzi ya azimio la JUNE mosi

Umati wa wanachama wa klabu ya Yanga wakiwa katika mkutano mkuu.

Uongozi wa klabu ya soka ya Yanga umewataka wanachama wake wote walio hai kujitokeza makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Twiga na Jangwani ili kutoa maoni yao kuhusu maazimio ya mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Juni Mosi mwaka huu na wanachama wa klabu hiyo kukubaliana kuuongezea muda uongozi wa klabu hiyo ili uweze kumalizia baadhi ya mambo muhimu ya kimikataba

Afisa habari wa timu hiyo Baraka Kizuguto amesema kumekuwa na tarifa na kelele za wanachama mbalimbali kupitia vyombo vya habari wakipinga maazimio ya mkutano huo na hivyo sasa klabu hiyo inaweka daftari la reja ili wanachama wajiorodheshe majina yao na namba za kadi zao na ikifikia idadi kama ya mkutano mkuu basi uongozi utabadilisha maamuzi hayo na kuitisha mkutano mwingine kwaajili ya kupanga upya masuala ya mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo.

Aidha Kizuguto amesema kwakuwa katika suala kama hili kuna baadhi ya wanachama watakuwa wakipinga maamuzi ya wanachama wenzao basi wao kwakuzingatia haki ya kidemokrasia ya kikatiba ya wanachama wake wameliomba jeshi la polisi nchini kuja kuweka ulinzi klabuni hapo ili kusiwepo na uvunjwaji wa amani na zoezi hilo la siku tano litakaloanza Jumatatu hadi Ijumaa limalizike kwa utulivu.