Watakaokosekana Atletico Madrid v Chelsea

Jumanne , 23rd Feb , 2021

Klabu ya Chelsea itamkosa mlinzi wake wa kati mbrazil Thiago Silva, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid, hatua ya 16 bora mchezo utakaochezwa nchini Romania. Amethibitisha kocha Thomas Tuchel.

Thiago Silva

The Blues wanacheza dhidi ya Atletico Madrid ya Hispania kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 bora, mchezo huu utachezwa Saa 5:00 usiku. Atletico ndio wenyeji japo mchezo huu unachezwa nchini Romania kutokana na vizuizi vya kujikinga na Corona vilivyowekwa nchini Hispania kutoka kwa wageni kutoka nchini England.

Kuelekea mchezo huu, Chelsea itamkosa Thiago Silva pekee miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza, mlinzi huyo aliumia kwenye mchezo dhidi ya Tottenham Februari 4, na amekosa michezo 4 kutokana na majeraha hayo, Tammy Abraham ambaye alionekana kupata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Southampton amesafiri na kikosi pamoja na Kai Havertz na Christian Pulisic.

Kocha wa Atletico Diego Simeone ataikosa huduma ya Jose Gimenez, Yannick Carrasco na Sime Vrsaljko. Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa msimu wa 2017-18 hatua ya makundi, ambapo Chelsea ilishinda mchezo mmoja kwa mabao 2-0 nyumbani kwa Atletico na mchezo mwingine ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dimba la Stanford Bridge.