Jumatano , 16th Jul , 2014

Mkuu wa msafara bwana Mwarami Mchume amesema kuachwa kwa wanamichezo hao kumetokana na tatizo la kiufundi llilitokea kwa waandaaji huko Scotland, lakini TOC inalifanyia kazi.

Wachezaji watatu wa judo kwenye timu ya madola waachwa.

Wachezaji watatu wa timu ya Tanzania itakayoshiriki michezo ya 20 ya Jumuiya ya Madola, wameachwa katika msafara ulioondoka alasiri ya leo kuelekea jijini Glasgow nchini Scoitland.

Mwalimu wa timu hiyo bwana Zaid Khamis amesema wamevunjwa moyo na tukio hilo na hawaelewi nini kilichotokea mpaka wachezaji wake watatu ambao wangeweza kurudi na medali kuachwa.

Katika kumuunga mkono mwalimu wake, mmoja wa wachezaji aliyebahatika kuondoka na timu hiyo bwana Geofrey Edward Mtawa amesema tukio hilo limewaathiri kiufundi na kisaikolojia kwani timu yao ilitengenezwa kwa misingi ya wachezaji saba kufanya mazoezi ya pamoja hivyo kupungua kwa hao watatu kumewaharibia mipango yao.

Lakini meneja wa timu hiyo ambaye ni mkuu wa msafara bwana Mwarami Mcheme alielezea mkasa mzima uliopelekea kuachwa kwa wapambanaji hao kwamba waandaaji wa michezo hiyo wamewaengua wana judo hao kutokana na kutokidhi vigezo, lakini akaongeza kwamba hali hiyo hutokea katika michezo kama hii cha msingi ni kupeleka taarifa sahihi kitu ambacho kamati ya Olimpiki Tanzania inakifanyia kazi.

Wachezaji walioachwa ni Ahmed Said Magogo, Gervas Leonard na Masodu Kombo. Timu ina jumla ya wachezaji 36 na viongozi na makocha wanane na jana Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliikabidhi bendera kama ishara ya kuwaaga na kuwatakia kila la heri.

Michezo ya 20 ya Jumuia ya Madola inatarajiwa kuanza tarehe 23 mwezi huu mpaka tarehe tatu mwezi ujao jijini Glasgow nchini Scotland.
*****************************************88