Jumanne , 21st Apr , 2015

Kocha wa timu ya taifa ya mpira wa wavu wa ufukweni kwa wanawake, Nassor Shariff amesema anaamini timu yake itafanya vizuri katika mashindano ya kanda ya tano ya wanawake yanayotarajiwa kufanyika Mei 7 mwaka huu Mombasa nchini Kenya.

Akizungumza na East Africa Radio, Shariff amesema ameshaanza mazoezi na timu na anaamini wachezaji wake watafanya vizuri katika mashindano hayo ambayo ni ya kuwania kushiriki michuano ya Afrika inayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu, nchini Congo Brazzavvile.

Shariff amesema, japo imekuwa kawaida kwa timu za wavu ufukweni kushindwa kufanya vizuri kutokana na kukosa uzoefu hivi sasa anaamini timu yake itafanya vizuri kutokana na maandalizi waliyonayo pamoja na umakini na timu watakazokutana nazo.