Alhamisi , 21st Apr , 2016

Pamoja na kutolewa katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika Yanga imetupwa katika hatua kama hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ambapo wadau wameitaka kuitumia vema nafasi hiyo na kufuta makosa.

Kikosi kamili cha timu ya Yanga.

Wadau wa michezo nchini Tanzania wameitaka klabu ya Yanga kujipanga vema kama inataka kufanya vema katika michuano ya kombe la Shirikisho mara baada ya jana usiku kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Al Ahly katika mchezo mkali uliopigwa katika uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria ukiwa ni mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora.

Wito huo umetolewa hii leo na wadau hao wakati wakizungumzia mchezo huo wa jana ambao Yanga ilionesha kiwango cha hali ya juu japo matokeo hayakuwa upande wao.

Wadau hao wamesema kuteleza si kuanguka na kinachotakiwa hivi sasa ni kwa klabu ya Yanga kujipanga na kujiandaa kwa kiwango bora cha kimataifa ili kukabiliana na changamoto za michuano ya CAF.

Yanga mara baada ya kutolewa katika michuano ya klabu bingwa sasa itacheza mchezo mmoja wa mtoano wa hatua ya 16 bora ya kombe la shirikisho barani Afrika [CCC] ambapo kwa mujibu wa droo ya ratiba ya hatua hiyo iliyotolewa na CAF hii leo Yanga wataanzia nyumbani kwa kucheza na wawakilishi wa Angola timu ya Sagrada Esperança wiki ya Mei 6-8 mwaka huu na marudio ni Mei 17-18 mwaka huu.

Aidha wadau hao wamesema ni wazi Yanga wana nafasi kubwa ya kuvuka hatua hiyo kama klabu hiyo itajipanga vema na kujiandaa kikamilifu huku ikiwaheshimu wapinzani wao na kwa ubora ilionao kwa sasa wana uhakika kwa asilimia kubwa timu hiyo kuvuka kikwazo hicho kikubwa ni benchi la ufundi kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Al Ahly.