Alhamisi , 23rd Jun , 2016

Baada ya mvutano kati ya Yanga na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwamba mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Yanga dhidi ya TP Mazembe ichezwe lini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, sasa jibu ni Jumanne kama ilivyotangazwa awali na TFF.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya michezo yao.

Afisa habari wa TFF, Alfred Lucas ameendelea kusisitiza mechi hiyo itachezwa Jumanne jioni kama ilivyotangazwa awali, na si kama walivyotangaza na klabu ya Yanga kuwa itapigwa usiku ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi kujitokeza hasa ikizingatiwa ni siku ya kazi na pia siku ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limekataa ombi la Young Africans ya Dar es Salaam juu ya kubadili siku na muda wa mchezo dhidi ya T.P. Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika taarifa ya CAF iliyofika TFF imesema mchezo huo utafanyika Jumanne Juni 28, 2016 saa 10.00 jioni kama ulivyopangwa awali kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Young Africans kwa upande wao waliomba mchezo huo ufanyike Juni 29, 2016 saa 1.30 usiku.

Kadhalika, kikao cha maandalizi katika mchezo huo kiliochofanyika leo Juni 23, 2016 kimeagiza uongozi wa Young Africans kuwaelimisha mashabiki wao kukaa katika eneo la mazoea tofauti na mipango yao ya kutaka kukaa eneo lote la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo wa kuwania Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Young Africans ya Dar es Salaam, Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa watatu kutoka nchi tatu tofauti kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua ambao utachezeshwa na Mwamuzi Janny Sikazwe wa Zambia.

Sikazwe atasaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba. Kamishna wa mchezo huo atakuwa Celestin Ntangungira wa Rwanda. Pia mchezo huo utakuwa na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza.

Lakini kwaupande wao Yanga kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wao, Jerry Muro amesema: “Ni kweli.” na kubwa lilikuwa ni suala pia la usalama kutokana na kutokuwa na uhakika kama kweli kuna umeme wa uhakika.

“Mechi itachezwa Jumanne na si Jumatano, kuchezwa usiku inaonekana hatuna uhakika wa umeme,” alisema Muro.

“Pia hatuna uhakika wa jenereta, hivyo hatuwezi kuingia kwenye hasara au kujaribisha kitu cha hatari wakati tunajua tunaweza kupoteza pointi kwa kanuni za Caf.”

Hao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.

Kikosi cha Yanga kimeweka kambi mjini Antalya, Uturuki na kinatarajiwa kurejea nchini kesho usiku kwa maandalizi ya mwisho.
Kikosi kamili cha Yanga kilichopo kambini Uturuki ambacho kinatarajiwa kurejea Ijumaa usiku ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.

Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Godfrey Mwashiuya na Obrey Chirwa.

Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.

Msafara upo chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh.