Jumatatu , 25th Oct , 2021

Baada ya kikosi cha Simba kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Africa katika raundi ya kwanza na Galaxy Janweng ,aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji na mshauri wake Crecentius Magori wameonyesha kutofurahishwa na matokeo yaliyojitokeza katika mchezo wa jana.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji katika moja ya mchezo.

Kupitia mitandao ya kijamii, Mohammed Dewji ameandika kuwa ''Kwakuwa nimejiuzulu, sina nafasi ya kutoa uamuzi wowote Simba. Ninachoweza ni kutoa ushauri kwa Mwenyekiti na bodi kuchukua hatua kali kwa wale ambao wanawajibika kwa upotevu wa mechi.Hii haikubaliki.

Kwa upande wa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo ambaye kwasasa ndiye mshauri mkuu wa Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi, Crecentius Magori ameandika ''usaliti ni kitu kibaya sana, hakivumiliki'' huku akisisitiza jana ilikua ni siku ya kiza kinene katika historia ya klabu ya Simba.

Simba ambayo ilikuwa ikiongoza kwa mabao matatu kwa sifuri lakini walijikuta wakipoteza faida waliyokuwa nayo katika dakika 45 za kipindi cha mwisho cha mchezo huo kwa kuruhusu mabao matatu yaliyowaondoa mashindanoni.

Kufuatia viongozi hao wa juu kutoa malalamiko yao mitandaoni inaonyesha ndani ya Klabu hiyo mambo si shwari, na huenda kuna watu watawajibishwa katika eneo la utendaji.