Alhamisi , 16th Mar , 2023

Uongozi wa klabu ya Yanga, umesema fedha zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeongeza ari kubwa kwa wachezaji kuipigania timu yao.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Salehe ameyasema hayo wakati wa uchezeshaji wa droo ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam hatua ya robo fainali.

Amesema, kipindi cha nyuma timu yao ilikuwa inaishia hatua ya awali ya michuano ya Kimataifa, lakini sasa vijana wamekuwa na hamasa kubwa ya kuipigania nembo ya timu yao na kuongeza kuwa, “tunashukuru kwa hamasa hii, wachezaji wanapambana kuipatia timu matokeo mazuri uwanjani, tunashukuru kwa kila kitu kinachochangia ushindi wetu.

“Historia imebadilika na wakati huu tunaenda kwenye mechi ya mwisho wa wiki tukiwa na shauku kubwa ya kuona timu yetu inashinda mbele ya wageni wetu US Monastir, mchezo utakaopigwa siku ya Jumapili katika Uwanja wa Taifa wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam,” amesema

Klabu za soka za Yanga na Simba, imezidi kujizolea fedha  Rais Samia, aliyeahidi kununua kwa Shilingi Milioni 5 kila goli linalopatikana, wakati timu hizo zinaposhiriki michezo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.