Ijumaa , 25th Nov , 2022

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limevitaka vyama vya soka nchini vinavyosimamia ligi za Wilaya na Mikoa kuwatumia zaidi wachezaji vijana wenye umri chini ya miaka ishirini (U20) ili kusaidia kuibua , kuvitengeza, kuvikuza na kuviendeleza vipaji vya vijana wengi nchini

Hayo aliyasema Rais wa TFF  Wallace Karia   wakati akitoa hotuba yake mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 17 wa TFF uliofanyika Jijini Mwanza; moja kati ya malengo ya mkutano huo ni pamoja na kufanya tathimini katika utekelezaji wa mipango inaaksi na malengo ya TFF kwa kipindi cha mwaka mzima.

Akieleza kuhusu umuhimu wa ligi hizo kwa daraja la Wilaya na Mikoa Rais Karia alisema kuwa kumekuwa na kasumba ya kuwatumia wachezaji wakubwa na baadhi yao wanaotoka kwenye timu za madaraja ya juu ambao hupatiwa nafasi na kipaumbele kwenye ligi hizo jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi za Shirikisho katika kuendelea kuibua vipaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, na baadala yake kuendelea kuwatumia wachezaji wale wale ambao tayari wamekwisha tumika kwa muda mrefu.

Alisema kufanya hivyo ni kuwakosesha nafasi wachezaji chipukizi ambao hapo baadaye wanaweza kuwa na msaada mkubwa kwenye timu za Taifa. Hivyo, ameviagiza vyama vya mpira wa miguu nchini  hasa katika ngazi za Wilaya na Mikoa kuhakikisha ligi hizo zinatoa nafasi kwanza kwa wachezaji wa U20 kabla ya kuwatazama wengine.

Aidha, Rais Wallace Karia alieleza sababu za kufanyika kwa Mkutano huo wa kila mwaka mapema zaidi kuwa ni kutokana uwepo wa michuano mikubwa ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 20, 2022 huko Qatar. Alibainisha kuwa TFF imelitizama hilo kwa jicho la tatu kutokana na ukweli kuwa wadau wengi wa soka macho na masikio yao wameyaelekeza kwenye Kombe la Dunia; kwa hiyo, isingekuwa vema kugonganisha ratiba hiyo na jambo kubwa kama hilo la Mkutano Mkuu wa Shirikisho.

Hata hivyo,  Rais Karia aliweka wazi kuwa michezo ya Ligi Kuu ya NBC haitasimama kupisha Kombe la Dunia, baadala itaendelea kama kawaida kutokana na ukweli kwamba hakuna timu ya Ligi Kuu Tanzania yenye wachezaji wengi wanaotakiwa na timu zao za Taifa kama Kanuni za TFF na Bodi ya Ligi zinavyoelekeza. Hivyo, ratiba ya Ligi Kuu itaendelea kama ilivyopangwa na hakutokuwa na mabadiliko yanayotokana na uwepo wa michuano hiyo ya Dunia.

Mkutano Mkuu wa TFF wa namna hii hufanyika kila mwishoni mwa  Mwaka na hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. Mkutano huu kwa kawaida huhudhuriwa na wajumbe halali na viongozi wenye mwaliko maalum kutoka Taasisi za soka na Serikali pia.