Jumatano , 1st Mei , 2024

Mahakama ya Kimataifa ya Haki imetoa uamuzi dhidi ya kutoa amri ya dharura ya kuzuia mauzo ya silaha za Ujerumani kwa Israel.

Silaha za Kivita

Nchi ya Nikaragua iliwasilisha kesi hiyo, ikidai kuwa Ujerumani ilikiuka mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mauaji ya kimbari kwa kutuma vifaa vya kijeshi kwa Israel.Serikali ya Ujerumani imesema kuwa kesi hiyo haikuwa ya haki.

Berlin ni mshirika mkubwa wa Israel na muuzaji wa pili mkubwa wa silaha kwa nchi hiyo baada ya Marekani. Uamuzi wa mwisho unaweza kuchukua miaka mingi. Uamuzi wa leo ulikuwa juu ya hatua za dharura zinazopaswa kutekelezwa haraka.
Mnamo mwaka 2023 asilimia 30 ya ununuzi wa vifaa vya kijeshi vya Israel ulitoka Ujerumani.

Nikaragua imesema mauzo ya silaha za Ujerumani kwa Israel yameifanya kuwa na utata katika madai ya uhalifu wa kivita wa Israel.

Israel imekanusha madai ya mauaji ya kimbari na kusema kuwa vitendo vyake katika Ukanda wa Gaza vinalenga kuangamiza Hamas.
Nchi hiyo ya Amerika ya Kati iliwasilisha kesi hiyo mjini The Hague mapema mwezi Machi kuwataka majaji kutoa hatua za dharura za kuizuia Berlin kuipatia Israel silaha na msaada mwingine.

Pia imesema Ujerumani imekiuka mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mauaji ya kimbari kwa kusitisha ufadhili wa shirika la misaada la Umoja wa Mataifa, UNRWA.