Ijumaa , 31st Oct , 2014

Wanawake wajasiriamali nchini Tanzania, wametakiwa kujiunga na majukwaa ya wanawake wajasiriamali yaliyopo kwenye mikoa hususani ile ya mipakani, ili wapate fursa ya kubadilishana ujuzi wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika biashara zao.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Wajasiriamali Wanawake nchini Tanzania (TWCC) Bi. Suzan Mtui.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Wanawake Wajasiriamali nchini Tanzania - TWCC Bi. Suzan Mtui, amesema hayo leo wakati akizungumzia uanzishwaji wa Jukwaa la wajasiriamali wanawake la Horohoro mkoani Tanga, Jukwaa ambalo mara litakapoanzishwa katikati ya wiki ijayo, litakuwa msaada mkubwa kwa ukuaji wa biashara za wajasiriamali wanawake wanaotaka kuuza bidhaa zao katika nchi jirani ya Kenya.

Kwa mujibu wa Bi. Mtui, Jukwaa hilo litawakutanisha akina mama wajasiriamali kutoka mkoa wa Tanga na ile ya jirani, ambapo ametaja moja ya changamoto zitakazotatuliwa kutokana na kuwepo kwa Jukwaa hilo kuwa ni namna ya kufanya biashara nje ya nchi, umuhimu wa vifungashio, upatikanaji wa taarifa muhimu za masoko pamoja na vibali vya mipakani na vile vya kufanya biashara nje ya nchi.

Mkutano wa uundwaji wa jukwaa hilo utafanyika Jumatano wiki ijayo na kwamba baada ya mkutano huo wa Tanga, TWCC itakutana na viongozi wa majukwaa kutoka mikoa yote ya Tanzania kwa lengo la kutoa mafunzo ya uongozi kwa viongozi hao ili wawe msaada kwa wanachama wao hasa umuhimu wa kukuza biashara zao.

Aidha, amesema tangu chemba hiyo ianzishwe miaka miwili iliyopita, biashara zinazomilikiwa na wanawake zimeongezeka na kupata masoko makubwa ndani na nje ya nchi, kwani idadi kubwa ya wanawake wajasiriamali hivi sasa wana ujuzi wa kutafuta masoko pamoja na mbinu za uzalishaji wa bidhaa zenye ubora unaohitajika katika masoko.

Bi. Mtui amesema hata hivyo suala la vifungashio vyenye ubora limekuwa changamoto sio tu kwa wanawake peke yao, bali hata kwa wanaume kwani ukosefu wa vifungashio vyenye ubora limekuwa kikwazo cha upatikanaji wa masoko mazuri ya bidhaa za wajasiriamali hapa nchini.