Jumanne , 2nd Apr , 2024

Moto ambao chanzo chake hakijajulikana umezuka katika nyumba ya Mathias Jeremiah mkazi wa mtaa wa 14 Kambarage kata ta Buhalahala Halmashauri ya mji wa Geita na kuteketeza baadhi ya vitu vya ndani ambavyo thamani yake hajafahamika.

Majirani waliokuwa karibu na Nyumba hiyo wamesema walisikia sauti ikiomba msaada nyakati za saa nne asubuhi katika Nyumba hiyo ambayo ilikuwa ikiwaka moto na ndipo walipoanza jitihada za kuzima moto na kupiga simu kitengo cha zimamoto na uokoaji.

“Nilipofika eneo la tukio nilikuta moto unawaka wananzengo wameshafungua visima wanachota maji kuzima ule moto uliokuwa unawaka vimeungua vyumba kama vitatu na vitu vilivyokuwemo lakini chamsingi sana nashukuru sana hakuna mtu yeyote aliyedhurika mwenye familia na watoto wake wote wapo salama kulikuwepo na gari wananchi wakalitoa na baadhi ya vitu vya sebuleni wakaviondoa visiungue kwakweli tunashukuru kwa ushirikiano wa Nzengo yetu” amesema Lukas Jeremiah ambaye ni ndugu wa mwenye Nyumba

“Nilikuwa nyumbani watoto wangu wakaja wanakimbia wakaniambia nyumba ya baba mdogo inaungua na mimi ikabidi nianze kukimbia kwenda eneo la tukio na kweli nilivyofika nikakuta moto unawaka lakini wananchi wapo wanazima moto”CHARLES PETRO-Mkazi wa 14 kambarage

“Mimi mtoto wangu ndo aliniambia njoo mama mama jera anaunguliwa nikauliza na nini akaniambia nyumba yake nikaja nikafika kweli nikakuta moto unawaka nikaanza kuhangaikia namba za zima moto kwenye simu zimo ila kwa kiwewe hatuzioni” Leah Yusuph Kengele - Mkazi wa 14 kambarage

Mama mwenye  nyumba hiyo Salah Mathias amesema wakati tukio hilo linatokea yeye alikuwa ameenda sokoni na nyumbani alimwacha dada wakazi akiendelea na shughuli za nyumbani.

“Nilikuwa nimetoka nikaenda sokoni nilipata taarifa narudi kufika nikakuta moto unawaka binti yangu wa kazi nilivyomuuliza akaniambia ulitokea moshi na ghafla moto ukaanza kuwaka kwaiyo hilo ndo tatizo” Salah Mathias-Mama Mwenye Nyumba

Afisa habari na mawasilino kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Geita Sagernt Bahati Lugodisha amesema baada ya kupokea taarifa walifika eneo la tukio na kuanza kuzima moto zoezi lililochukua dakika 15 huku akisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kujua chanzo halisi cha tukio hilo

“Chanzo cha Tukio mpaka sasa hivi hakijajilikana wataalamu wetu maana ya investigation ofisa wanaendelea na uchunguzi na uchunguzi ukikamilika tutawajulisha wananchi nini kimesababisha huo moto” - Sagernt Bahati Lugodisha - Afisa habari jeshi la zimamoto na Uokoaji Geita

Habari nzima na video ya tukio hili usikose #EATVSAA1 leo kuanzia saa moja jioni #EATV