Jumatatu , 23rd Feb , 2015

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekiri kuwakamata viongozi wa Umoja wa Wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT, ambao wamekuwa wakitaka kuandamana kwenda Ikulu.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekiri kuwakamata viongozi wa Umoja wa Wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT, ambao wamekuwa wakitaka kuandamana kwenda Ikulu kumuona Rais kulalamikia kile walichodai kuwa ni kutopatiwa ajira mara baada ya kuhitimu mafunzo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, amewataja viongozi hao kuwa ni Katibu wa Umoja huo Linus Emmanuel pamoja na Mwenyekiti wake Bw. George Galus Mgoba, ambaye wiki iliyopita alidai kutekwa na baadaye kuonekana akiwa amejeruhiwa.

Kamishna Kova amesema kukamatwa kwa viongozi hao kunakwenda sambamba na kupiga marufuku mikusanyiko na shughuli zozote walizopanga kuzifanya, kutokana na madai yao kuwa ni kinyume na kiapo walichotoa wakati wa kuhitimu na pia zinalenga kufanya makosa ya uchochezi.