Jumanne , 10th Jun , 2014

TFF/CAF waahidi kozi zaidi kwa makocha Tanzania lengo likiwa ni kuhakikisha Tanzania inaondokana na kilio cha waalimu wenye taaluma ya madaraja ya juu ya ualimu wa mpira wa miguu

Baadhi ya walimu wa soka wakiwa katika moja ya semina za mafunzo kutoka CAF.

Kozi ya makocha wa mpira wa miguu ya Leseni B inayotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeendelea hii leo kwenye hosteli za TFF zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

Kozi hiyo ya wiki mbili inashirikisha makocha zaidi ya 20 wenye Leseni C kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kozi ambayo inaendeshwa na wakufunzi wa CAF, Sunday Kayuni pamoja na mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi.

Ambapo mkufunzi mkuu Salum Madadi amesema kozi hiyo ni muhimu kwa makocha hao na itawasaidia sana hasa katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa ligi mbalimbali na wataendelea kufanya kozi nyingi iwezekanavyo ili kupata walimu wengi wenye taaluma ya ukocha daraja la juu.

Kwa upande wao baadhi ya makocha wanaohudhuria kozi hiyo Denis Kitambi kocha wa Ndanda FC ya Mtwara iliyopanda daraja msimu huu na Meck Mexime Kocha wa Mtibwa sugar ya Morogoro wamesema kozi hiyo itawasaidia sana kuongeza ujuzi zaidi katika kazi zao za ufundishaji katika vikosi vya timu zao ambavyo vitakabiliwa na michuano ya ligi kuu bara msimu ujao unaoanza August mwaka huu.