Jumatatu , 28th Mar , 2016

Shirikisho la ngumi nchini Tanzania BFT linatoa wito kwa wadau na Watanzania wote na Serikali kwa ujumla kuisaidia timu ya taifa ya ngumi ya Tanzania isafiri kwenda nje kushiriki mashindano yakusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Olimpiki ya Rio.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya ngumi ya Tanzania wakiwasili baada ya kutoka nje walikoenda kushiriki moja ya mashindano.

Baada ya kukosa kushiriki michuano ya kufuzu kwa mashindano ya Olimpiki ya Rio Brazil yaliyofanyika mwanzoni mwa mwezi huu nchini Cameroon kwa upande wa bara la Afrika timu ya taifa ya ngumi ya Tanzania ambayo imevunja kambi kwa muda sasa inanafasi nyingine yakwenda kushiriki michuano ya mwisho ya kushiriki mchujo wa kwenda Brazil.

Timu hiyo ilishindwa kwenda katika michuano hiyo dakika za mwisho baada yakukosa nauli na pesa za matumizi mengine wakiwa huko ugenini kwa muda wote wa mashindano hayo yaliyofanyika huko jijini Younde jambo ambalo sasa limelifanya shirikisho la ngumi nchini Tanzania BFT kutoa wito kwa wadau kuisaidia kwa nguvu zote timu hiyo iliikatafute fursa hiyo kwenye michuano ijayo ya kufuzu itakayofanyika June mwaka huu nchini Azabeijan.

Katibu mkuu wa BFT Makore Mashaga amesema hayo wakati akithibitisha uwezekano wa timu hiyo kupata nafasi ya mwisho ya kwenda kushiriki michuano ya kufuzu baada ya awali kukosa nafasi ya kushiriki hatua hiyo kwa upande wa bara la Afrika michuano iliyofanyika jijini Younde Cameroon.

Mashaga amesema michuano hiyo ya kufuzu ya Azabeijan ni kwa mataifa toka mabara yote hivyo ni wazi itakuwa ni migumu mno kwakuwa kwanza ndiyo itakuwa ya mwisho kwa washiriki kusaka tiketi ya kwenda Rio Brazil katika michuano ya Olimpiki itakayofanyika mwanzoni mwa mwezi wa nane mwaka huu.

Akimalizia Mashaga amesema itakuwa ni aibu na jambo la fedheha kwa nchi kama timu hiyo itashindwa kwenda katika michuano hiyo ya kufuzu hivyo ni vema kwa wadau wote ikiwemo Serikali kuhakikisha wanaipasapoti timu hiyo katika maandalizi yake kwa muda huu uliobaki na pia kufanikisha safari ya timu hiyo na akakumbusha kuwa timu hiyo ni ya Watanzania wote na si vyema majukumu hayo yakaachwa kwa chama ama shirikisho husika la ngumi na ndiyo maana safari ya kwenda Cameroon ilikwama kutokana na mapungufu hayo.