Jumatano , 30th Mar , 2016

Kocha mkuu wa kikosi cha timu ya soka ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys Bakari Shime amesema timu hiyo ikipata udhamini na misaada ya kutosha basi ni wazi itafanya maandalizi ya kutoka ikiwemo kuweka kambi nzuri.

Kikosi cha timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 cha Tanzania [Serengeti Boys].

Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya soka ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys Bakari Shime amesema timu hiyo ikipata udhamini na misaada ya kutosha basi ni wazi itafanya maandalizi ya kutosha ikiwemo kuweka kambi nzuri.

Akizungumza kwa niaba ya benchi la ufundi la kikosi cha timu ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania Serengeti Boys kocha Shime amelipongeza Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) kwa fanikisha kuipatia timu hiyo michezo ya kirafiki dhidi ya timu ngumu ya vijana ya Misri.

Shime ambaye aliwahi kuwa kocha mkuu wa maafande wa JKT Mgambo kutoka Tanga amesema michezo hiyo ni muhimu sana kwao ili kujua mapungufu ya kikosi hicho ambacho kinaendelea na mazoezi katika uwanja wa Karume, na sasa ni fursa kwa wadau nao kuunga mkono juhudi za TFF.

Shime amesema ili timu hiyo imeweze kufanikiwa katika malengo waliojiwekea njia pekee ni kwa Watanzania wote kujitoa kwa hali na mali kwa moyo wote ili kuisaidia katika maandalizi yake na pia kuwezesha na kufanikisha kwa namna moja ama nyingine timu hiyo kupata michezo mingi ya kirafiki ya kimataifa na timu za vijana wenzao kutoka nchini zilizokatika viwango vya juu vya ubora wa soka Afrika na duniani kwa ujumla.

Aidha, Shime ambaye anasaidiana na kocha msaidizi wake Sebastian Mkomwa wakishauriwa na Kim Poulsen, amesema michezo migumu kama hiyo dhidi ya Wamisri hao itasaidia kujua ni kwa kiasi gani kambi yao ya mazoezi waliyoianza takribani wiki moja iliypoita imefanikiwa kwa kiasi gani na mapungufu yako wapi wayafanyie kazi mapema kabla ya mchezo wa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwaka 2017 nchini Madagascar.

Shime amesema timu hiyo ambayo leo asubuhi katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam itacheza mchezo wa kujipima nguvu na timu ya vijana ya klabu ya Azam FC inahitaji sapoti ya nguvu na udhamini kwani vijana hao wameonyesha uwezo na wana hari na pia kuwaandaa mapema kwani wao ndiyo timu ya taifa ya wakubwa ya baadaye na kitendo cha kuliachia shirikisho peke yake ni sawa na kuwatelekeza vijana hao ambao wamejitoa kuipeperusha bendera ya taifa.

Tanzania itaanza kuwania kufuzu kwa fainali hizo mwishoni mwa mwezi Juni, kwa kucheza dhidi ya timu ya soka ya taifa ya Vijana ya Ushelisheli.