Ijumaa , 4th Mar , 2016

Ikiwa imepita takribani wiki moja tangu bondia Mtanzania Francis Cheka maarufu kama [SMG] ameendelea kupokea pongezi mbalimbali kutoka kwa wadau na mashabiki wa michezo nchini hii ni baada ya hii leo kupokea pongezi kutoka Serikali ya Tanzania.

Waziri wa habari utamaduni sanaa na michezo Nape Nnauye akimkabidhi cheti bondia Francis Cheka.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imempongeza na kumtunuku cheti cha kuthamini ushindi wa ubingwa wa mabara wa WBF alioupata hivi karibuni bondia Francis Cheka katika pambano la raundi 12 uzito wa kati kwa kumpiga kwa pointi bondia Geard Ajetovic wa Serbia.

Cheka alifanikiwa kuibuka na ushindi huo katika pambano hilo mara baada ya kufanikiwa kupiga masumbwi yaliyomfikia kwa wingi mpinzani wake huyo ambaye makazi yake yako nchini Uingereza na hivyo kujizolea alama nyingi toka kwa majaji waliosimamia mchezo huo na hatimaye kutawazwa bingwa mpya baada ya kutwaa mkanda wa ubingwa wa mabara wa WBF .

Wakizungumza wakati wa makabidhiano hayo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye amempongeza Cheka kwa ushindi huo muhimu kwa taifa na kumkabidhi cheti hicho mahususi kwa ushindi huo na kutambua mchango wake katika kuipeperusha vema bendera ya taifa katika medani ya michezo kimataifa.

Waziri pia amemuahidi Cheka na wanamichezo wengine kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za wanamichezo wanaofanya vizuri.

Kwa upande wake Francis Cheka mwenyewe akiwa na mdogo wake Cosmas Cheka ambaye naye alitwaa mkanda wa ubingwa wa Afrika wa WBF pamoja na kukabidhi mikanda yao ya ubingwa wa WBF ameishukuru serikali na watanzania wote kwa ujumla kwa kuwaunga mkono tangu kuanza maandalizi hadi siku ya pambano hilo.

Pia ametoa pongezi maalum kwa waandishi wa habari kwa kutangaza habari zote za pambano hilo tangu mwanzo hadi hivi sasa wakati wa mwendelezo wa utoaji pongezi na zawadi mbalimbali kutoka kwa wadau mbalimbali wa michezo kutokana na ushindi huo.

Kwa upande mwingine Rais wa Oganaizesheni ya ngumi za kulipwa nchini Tanzania TPBO Yasin Abdalah Ustadhi ametangaza rasmi kuwa kwa ushindi aliopata Cheka, anapata nafasi ya kucheza mpambano wa ubingwa wa dunia ama kutetea ubingwa wake wa WBF kwa kucheza na bondia bingwa kutoka nje ya nchi.