Jumamosi , 11th Jun , 2016

Baada ya kupita kwa takribani miaka miwili bila kuwepo kwa mashindano ya tenisi kwa vijana wadogo katika klabu ya Dar Gymkhana hatimaye safari hii watoto wamefurahia shindano hilo kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam.

Moja ya viwanja vya mchezo wa Tenisi pamoja na vifaa vya mchezo huo.

Zaidi ya wanamichezo 40 vijana wa umri chini ya miaka 6 hadi 18 kutoka mikoa ya Arusha, Morogoro, Pwani na wenyeji Dar es Salaam wanashiriki katika michuano ya vijana inayofanyika katika klabu ya Dar Gymkhana jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo ya siku mbili yameanza na yanahusisha vijana wa kike na kiume ambao wanachuana kwa mtindo wa mtoano na fainali zake zinataraji kupigwa hapo kesho.

Akizungumzia shindano hilo mratibu wake bi Inger Njau amesema lengo kwanza ni kuamsha hali ya vijana kuupenda na pia kuwarejesha vijana hao mchezoni baada ya kuwa nje ya kimashindano kwa muda mrefu, lakini pia kuwapa uzoefu na changamoto za kimashindano ili kuwaweka tayari kwa michuano ya kimataifa ya ndani na nje ambayo itafanyika siku zijazo.

Njau amesema mgawanyiko baina ya wadau wa mchezo huo ndiyo moja ya changamoto kubwa ya mchezo huo kuanza kushuka kwa kasi na kupelekea kushindwa kufanyika kwa mashindano mbalimbali makubwa ya ndani kutokana na kukosekana kwa umoja na ushirikiano katika kufanikisha na kuratibu michuano hiyo kwa sasa.

Ikumbukwe kwa sasa chama cha tenisi nchini kimebakiwa na viongozi wawili katibu mkuu na mjumbe wa kamati ya ufundi kufuatia viongozi wengine wote wa juu na wajumbe kuachia ngazi kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa ndani wa wao kwa wao ambao umepelekea kutokea kwa mgawanyiko na hatimaye wakaachia ngazi.

Mama Njau amesema mgogoro na hali ya msuguano baina ya viongozi wa chama cha mchezo wa tenisi Tanzania TTA imekuwa ni kikwazo cha kufanyika kwa mashindano mbalimbali ya mchezo huo hasa kwa vijana, jambo lililopelekea vijana wengi wadogo kushindwa kuendelea ama kuamua kuacha kujihusisha na mchezo huo.

Njau ambaye ni mdau mkubwa wa mchezo wa tenisi ambaye ni mratibu wa michezo ya tenisi kwa watoto amesema ili mchezo huo uweze kurejea katika hadhi yake ni wazi viongozi wa mchezo wa tenisi waliosalia kwa sasa wanapaswa kujifunga kibwebwe na kutafuta udhamini na pia kuwa mstali wa mbele kushawishi uwekezaji mkubwa katika mchezo huo kwa ngazi zote.

Njau amemaliza kwa kusema kuwa kutokana na uchungu alionao kwa watoto hasa wanaocheza mchezo huo ndio maana akaamua kuwaandalia shindano hilo maalumu na hii amesema sio mwisho pia anataraji kuandaa shindano jingine katikati ya mwezi wa tisa na pia mwishoni mwa mwaka huu na anachoomba ni ushirikiano kwa wadau wote wa michezo na pia wanatenisi wote kwa ujumla.